HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 29, 2019

Kina Simbu wastuliwa kimtindo Qatar

Mwanariadha maarufu Tanzania, Alphonce Simbu (kulia), akijifua jijini Arusha ikiwa ni maandalizi ya kushiriki mashindano ya Dunia yanayoendelea Doha, Qatar. (Na Mpiga Picha Wetu).


NA MWANDISHI WETU

BAADA ya Tanzania kuanza vibaya katika mashindano ya Riadha ya Dunia ‘IAAF World Championships 2019’ jijini Doha, Qatar, wanariadha wanne waliosalia wameshtuliwa wajiandae kisaikolojia kwani hali ya hewa huko ni balaa.

Usiku wa kuamkia Septemba 28, Tanzania ilianza kutupa karata yake katika mbio za Marathon kwa wanawake na mwakilishi wake, Failuna Matanga kuchemsha.

Failuna kutoka Klabu ya Talent jijini Arusha, ambaye alikuwa akipigiwa chapuo kuitoa Tanzania kimasomaso, alishindwa kumaliza Kilomita 42.195 na kuishia Kilomita 21, alipojitoa akiwa ametumia saa 1:11.25 kutokana na kushindwa kuhimili hali ya joto kali iliyoko huko.

Baada ya Failuna, sasa Tanzania imebakiwa na wachezaji watatu wote katika Marathon, wakiongozwa na Mshindi wa Medali ya Shaba katika mashindano yaliyopita huko London, Alphonce Simbu wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), Agustino Sulle kutoka Klabu ya Talent na Stephano Huche wa African Ambassador Athletics Club (AAAC).

Akizungumza kwa simu kutoka Doha jana, Kiongozi wa timu ya Tanzania, Wilhelm Gidabuday, alisema hali ya hewa ni ya joto kali, ambalo linawaathiri wanariadha wa mataifa mbalimbali kama ilivyotokea kwa Failuna.

“Kwanza nimpongeze Failuna kwa kile alichojitahidi kukifanya, amekuwa mpiganaji wa kwanza kuingia kwenye uwanja wa vita na ingawa hakuweza kutupa medali lakini ametupa mbinu ya vita…Nimeongea naye na ameniomba niwaambie wenzake waliobaki nyumbani kwamba, waanze kujiandaa kisaikolojia kupambana na hali iliyoko huku,” alisema Gidabuday ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), na kuongeza:

“Simbu na wenzake wanapaswa kwa siku hizi chache zilizobaki, wajiandae kukabiliana na hali ya hewa ya huku ikiwamo kunywa maji mengi.”

Gidabuday, aliwaomba Watanzania kutovunjika moyo kwa kilichotokea kwa Failuna, bali wazidi kuwaombea wapambanaji waliosalia na mapambano yanaendelea.

Wanariadha waliosalia, wanatarajiwa kuondoka nchini Oktoba 2 mwaka huu, kabla ya kuingia kwenye kinyang’anyiro Oktoba 5.

No comments:

Post a Comment

Pages