*Waziri Mkuu asema wasiotaka kuelewa Serikali itashughulika nao
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewaonya watu wote wakiwemo wafanyabiashara
wasiokuwa waaminifu ambao wanajihusisha na utoroshaji wa madini, waache
mara moja, Serikali ipo makini imejidhatiti vya kutosha na kwamba
haitokuwa na huruma dhidi yao.
Serikali
imefuta kodi ya ongezeko la thamani (VAT-18%) na kodi ya zuio
(withholding tax-5%) kwa wachimbaji watakaouza madini kwenye masoko
yalioanzishwa nchini ikiwa ni mikakati ya kuwaendeleza wachimbaji wadogo
ili waweze kuongeza uzalishaji na hivyo kujiongezea tija na kuchangia
katika pato la Taifa.
Waziri
Mkuu ametoa onyo hilo leo (Jumapili, Septemba 22, 2019) wakati
akifungua maonesho ya Teknolojia na Uwekezaji katika Sekta ya Madini
yanayofanyika kwenye uwanja wa CCM Kahangalala mjini Geita. Amesema kwa
wale wasiotaka kuelewa na kuacha kutorosha madini Serikali itashughulika
nao.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itaendelea kutatua changamoto wanazokutana nazo
wachimbaji wadogo ikiwemo matumizi ya teknolojia duni katika uchimbaji
na uchenjuaji madini. “Nitoe wito kwa wadau kuitumia fursa ya uwekezaji
kwa kuanzisha biashara ya vifaa vya uchimbaji na uchenjuaji nchini.”
Pia,
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wadau wa madini kuwa
katika mkutano wa 16, wa Bunge la 11 lilijadili na kuridhia Azimio la
Kuridhia Mkataba wa Minamata kuhusu kupunguza kwa kadiri iwezekanavyo
matumizi ya zebaki ifikapo 2030.
Amesema
lengo la mkataba huo ni kuanza kupunguza na hatimaye kuacha matumizi ya
zebaki kwenye uchenjuaji wa dhahabu hususan kwa wachimbaji wadogo. Kwa
mantiki hiyo, amewasihi wachimbaji wadogo kuepuka matumizi ya zebaki
katika uchenjuaji na kuanza kutumia njia nyingine zilizopo.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amesema kwa kipindi kirefu kumekuwepo na changamoto ya
wachimbaji wadogo kufanya shughuli za uchimbaji bila kuwa na taarifa
sahihi za kijiolojia, hivyo kusababisha wachimbaji wengi wadogo
kuchimba kwa kubahatisha na hata wengine kutumia imani za kimila katika
kuchagua maeneo ya uchimbaji.
“Kwa
msingi huo, nawahimiza wadau mbalimbali katika Sekta ya Madini hususan
wachimbaji wadogo kuitumia kikamilifu Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini Tanzania (GST) ili kupata taarifa muhimu na sahihi za kijiolojia
pamoja na ushauri wa kitaalamu katika utafutaji wa madini.”
Amesema
sambamba na kutenga maeneo kwa ajili ya wachimbaji wadogo kwa
kuzingatia taarifa za kijiolojia kupitia GST na STAMICO, Serikali
imeendelea kuandaa machapisho yenye kuonesha maeneo yanakopatikana
madini nchini.
Waziri
Mkuu amewataka wachimbaji wadogo kutumia fursa ya uwepo wa taasisi
hiyo ili kuepuka kuwekeza fedha zao nyingi katika maeneo ambayo hayana
madini na hivyo, kufanya kazi kwa kubahatisha jambo ambalo halina tija
kwao na Serikali kwa ujumla.
Amesema
Serikali imeanzisha vituo vya umahiri na vituo vya mfano kwenye baadhi
ya maeneo nchini kwa ajili ya kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu masuala ya
madini kwa wachimbaji wadogo, pia vituo hivyo, vitatumika kufanya
maonesho ya madini na vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchimbaji
madini.
Kaulimbiu
ya maonesho hayoinasema ‘Madini ni Chachu ya Ukuaji wa Uchumi wa
Viwanda’ Tuwekeze kwenye Teknolojia Bora ya Uzalishaji na Tuyalinde
Masoko ya Madini.
Amesema
kaulimbiu hiyo inakwenda sambamba na maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2015/2020 ambayo pamoja na mambo mengine
inaielekeza Serikali kusimamia na kuhakikisha uwekezaji katika shughuli
za kuongeza thamani madini ili kukuza mchango wa sekta hiyo kwenye Pato
la Taifa.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini Doto Biteko amesema kwa sasaSerikali na makampuni yanayomiliki migodi wanaheshimiana kwani makampuni hayo yanatii magizo na kufuata sheria za nchi.
Waziri
Doto amesema kabla ya kuåfunguliwa kwa masoko ya madini nchini
makusanyo ya dhahabu yalikuwa kilo 101 kwa mwezi hivi sasa baada ya
masoko kufunguliwa makusanyo yameongezeka na kufikia kilo 1,974.
Hata
hivyo, Waziri huyo wa Madini amesema kwa sasa nidhamu ya Watanzaniua
katika kusimamia ununuzi na uuzaji dhahabu imevutia wauzaji dhahabu toka
nchi za jirani kwani hakuna tena wizi wala utapeli katika biashara
hiyo.
Hivyo,
Waziri huyo ameyataka makampuni yanayomiliki migodi kutoa tenda kubwa
kwa wazawa na makampuni ya ndani badala ya kuyapa makampuni ya nje na
kuzipa kampuni za ndani tenda ndogondogo.
No comments:
Post a Comment