HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 23, 2019

GGR kujenga kiwanda cha kusafisha dhahabu

NA MWANDISHI WETU

 
KAMPUNI ya Geita Gold Refinery Limited (GGR) inayomilikiwa na Watanzania inajenga kiwanda cha kisasa cha kusafisha dhahabu inayotoka kwa wachimbaji nchini.


Kampuni hiyo ilipewa leseni ya kusafisha dhahabu ambayo ni tayari kwa matumizi (RFL 001/2019) na Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini Julai 16, 2019.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa Mmoja wa Wakurugenzi wake, Sarah Masasi, kampuni hiyo itakuwa na uwezo wa kusafisha dhahabu inayofikia tani 100 kwa mwaka yenye ubora wa juu wa asilimia 99.99 inayojulikana pia kama 999.9 (999.9 fineness or Four-Nine Gold).


"Uzalishaji utakuwa kwa viwango vya juu vya kimataifa vitakavyothibitishwa na mamlaka husika za kupima viwango. Masuala yanayohusu usimamizi wa mazingira, pamoja na usalama wa wafanyakazi, yataendeshwa na kusimamiwa ipasavyo kwa viwango vya kimataifa," ilisomeka taarifa hiyo.


Mkurugenzi huyo alisema kiwanda hicho kitakuwa cha pili kwa ukubwa Afrika baada ya kiwanda cha aina hiyo kilichoko Afrika Kusini huku Afrika Mashariki kikiwa cha kwanza.


Masasi alisema kiwanda hicho kitaongeza nafasi za ajira na kukuza teknolojia ya kisasa itakayoongezea thamani ya madini ya dhahabu na hivyo kuongeza faida yake kwa taifa.


“Juzi tulishiriki katika maonesho ya dhahabu yaliyofanyika kwa mara ya pili jijini Geita na kutoa melezo kuhusu mpango wetu huu mbele ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa,” alisema.


Masasi alisema kiwanda hicho, kitakuwa na uwezo wa kuzalisha dhahabu ya madaraja ya juu inayotambuliwa kimataifa kama vile miche ya adhahabu ya kilo moja moja na miche ya aunzi 400 (400 troy-ounce bars).


Alisema kiwanda kitakuwa na chumba cha kuhifadhia dhahabu ghafi cha kiwango cha juu kabisa duniani katika tasnia ya dhahabu (a 50-tonne UL certified Class-3 vault).


Mkurugenzi huyo alisema sehemu kubwa ya wamiliki wa kampuni hiyo ni Watanzania na kwamba wanawekeza ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono mkakati wa kitaifa wa kuelekea uchumi wa kati unaotegemea viwanda.

“Dhamira yetu ni kuongeza imani ya umma na ya kimataifa katika sekta ya madini ya Tanzania. Usafishaji wa madini utakaofanyika utasaidia kudhibiti utoroshaji wa dhahabu nje ya nchi kwa kuzalisha dhahabu itakayotambulika kimataifa kutokana na kuwa alama zote muhimu na nambari. Pia tunatumia teknolojia inayosaidia suala zima la utambuzi," ilisomeka taarifa hiyo.


Aidha, taarifa hiyo ya Masasi ilisema itawawezesha polisi na maofisa wa forodha kutambua haraka usahihi wa dhahabu iliyoidhinishwa kwa usafirishaji kama ni sahihi au siyo na pia ni rahisi kutambua dhahabu bandia kutoka Tanzania.


"Kiwanda hiki kitasaidia sana juhudi za kimataifa na za kikanda kuhusu usambazaji wa bidhaa za dhahabu zinazokidhi viwango na kitaongoza katika kudhibiti utakatishaji fedha unaopitia tasnia hii ya dhahabu,” ilisema taarifa.

Tanzania inatambulika kama moja ya wazalishaji wakuu wa dhahabu barani Afrika. Uanzishwaji wa kiwanda cha kusafisha dhahabu cha kisasa nchini kutachangia katika mpango wa Serikali wa kuongeza thamani katika vitu vinavyozalishwa hapa nchini.

No comments:

Post a Comment

Pages