HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 24, 2019

Tatoa yalia na ucheleshwaji wa mizigo bandarini

 Mwenyekiti wa Tatoa, Angelina Ngalula.


NA JANETH JOVIN

CHAMA cha Wamiliki wa Magari ya Mizigo (Tatoa) kimesema kumekuwepo na changamoto ya wasafirishaji kuchelewesha mizigo kutokana na foleni zinazosababishwa na taasisi zinazoruhusu mizigo kutoka bandarini kushindwa kufanya kazi kwa umoja hali iliyosababisha wasafirishe mizigo tani Milioni 5.1 wakati mahitaji yakiwa  tani Milioni 20.

Aidha Tatoa kimesema changamoto hiyo pamoja na ya foleni ya malori bandarini na mipakani inasababisha pia sekta hiyo kushinda  kuhudumia vyema soko la Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc).

Hayo yamebainishwa mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tatoa, Angelina Ngalula, wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa chama hicho.

Alisema licha ya Serikali kufungua milango katika soko la Sadc bado wasafirishaji wanakabiliwa na changamoto ya ucheleshwaji wa mizigo kutoka bandarini inayosababishwa na  foleni inayotokana na taasisi zinazoruhusu mizigo kutoka bandarini kushindwa kufanya kazi kwa umoja.

Alisema Sekta ya usafirishaji bado haijaweza kuhudumia watu kwa asilimia 75 kutokana na uwepo wa foleni hiyo ya kutoa mizigo bandarini inayokuchukua hadi saa nane kufika umbali wa Kilometa mbili na foleni katika maeneo ya mipaka kama Tunduma.

Ngalula alisema kama changamoto hiyo ingetatuliwa wangeshika nafasi ya kwanza kwa kuiingizia Serikali fedha za kigeni kutoka nafasi ya pili wanayoshikilia sasa.

Alisema mwaka 2017 waliingizia Serikali Dola za Marekani bilioni 1.14 na mwaka 2018 ziliongezeka na kufika Dola za Marekani bilioni 1.20.

"Mambo tunayojiuliza ni soko lililopo, fursa zilizopo, vikwazo vilivyopo, mapendekezo yetu na mambo yatakayotatuliwa yatasaidia vipi kupambana kuweza kuishinda sekta ya utalii inayoongoza kwa kuiingizia Serikali fedha za kigeni," alisema.

Aidha, Ngalula aliiomba Serikali kuunganisha tozo zote zinazohusisha magari ya kusafirisha mizigo ili kuondoa usumbufu kwa madereva kuchelewesha mizigo ya wateja.

Naye , Waziri wa Ujenzi,  Uchukuzi na Mawasiliano Isack Kamwelwe, alisema  Serikali ilishatoa maagizo kuwa, wadau wote wanatakiwa wakae ofisi moja kwa ajili ya kufanya kazi kwa pamoja na kuondokana na changamoto zote za foleni za mizigo bandarini.

"Watendaji wote wakae jengo moja kama mmoja akikwama wajue wanamsaidiaje na ufahamike ni ofisi gani imekwamisha mzigo kutoka bandarini na ikiwezekana apige simu makao makuu ya ofisini yao aseme kuwa amekwama na kama ni shida ya mtandao wautekenye huko ukae sawa," Kamwale alisema.

Aidha, aliwataka wamiliki wa malori, kununua mabehewa na vichwa vya treni ili Tatoa nao waweze kuhudumia sekta ya usafiri wa reli wakati ujenzi wa reli ya kisasa ya SGR ukiendelea.

"Tunataka reli ya Tazara ibebe tani milioni 5 kwa mwaka na zinazobebwa kwa sasa siwezi kuzitamka. Naomba nyie Tatoa nanyi msimiliki tu malori mnunue na mabehewa na vichwa vya treli ili sasa nanyi msafirishe mizigo kwa njia ya reli," Kamwelwe alisema.

kuhusu tozo, alisema sekta ya usafirishaji zipo zaidi ya 40 ambazo zote ameshaziainisha kwa ajili ya kuzifanyia kazi na watatoa mamaamuzi hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment

Pages