HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 24, 2019

Serikali yaondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi mipakani

NA JANETH JOVIN

SERIKALI kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara imesema kuwa imeondoa vikwazo vyote vya kikodi na visivyokuwa vya kikodi katika mipaka yote nchini  kwa lengo la kuhakikisha biashara mipakani zinaimarishwa na kufanyika kwa ufanisi zaidi.

Katika kufikia malengo hayo, Wizara hiyo imeutaarifu Umma na Wafanyabiashara hususan wale wanaofanya biashara mipakani kuwa, imeweka utaratibu maalum utakaowezesha kutoa taarifa juu ya vikwazo, changamoto au kero za kibiashara hasa zile zisizokuwa za kikodi (NTBs) wanazokumbana nazo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa wizara hiyo,  Stella Manyanya (pichani), alisema lengo la kuweka utaratibu huu ni kuwezesha wafanyabiashara kupata huduma haraka kupitia Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali zinazotoa huduma mipakani.

Alisema kwa kuanzia, Wizara hiyo imetoa anuani maalumu za barua pepe na namba za simu za watendaji ambazo watapenda kila mfanyabiashara anayepata vikwazo aweze kutoa taarifa kupitia namba hizo.

"Pia tunawataka wakuu wa taasisi walioko kwenye vituo vya mipakani kubandika orodha hiyo ya namba za simu kwenye mbao za matangazo ili kurahisha mawasiliano. Vikwazo visivyokuwa vya kikodi ni pamoja na rushwa ya kifedha na isiyo ya kifedha, urasimu na kutotoa miongozo ya taratibu zinazohitajika, kukosa taarifa muhimu na kutojua fursa zilizopo," alisema na kuongeza.

"Taarifa hizo zinapaswa kutumwa kwa Mratibu wa Vikwazo Visivyo vya Kiushuru (NTB’s)  Aneth Simwela kupitia barua pepe ifuatayo tanzania@tradebarriers.org au piga simu namba +255622259341," alisema Waziri Manyanya.

Aidha alisema kwa changamoto za masuala ya Viwanda na Masoko, Wafanyabiashara na Wadau wanaweza kuwasilisha changamoto zao kupitia barua pepe dawatilamsaada@mit.go.tz au kuwasiliana na Andrew Shirima wa Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia namba ya simu +255713500532.

Hata hivyo Waziri Manyanya alisema Wizara na Taasisi ambazo zinazotoa huduma mipakani ni pamoja na:
Mamlaka ya Mapato (TRA),  Idara ya Uhamiaji, Wakala wa Vipimo, Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA),  Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), Kitengo ya Huduma za Afya ya Mimea,  Idara za Maliasili na Utalii, Idara za Mifugo na Uvuvi Halmashauri za Wilaya na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade).

"Endapo hutaridhika na huduma kutoka taasisi yeyote tajwa hapo juu, wasilisha malalamiko yako kwa barua pepe minister@mit.go.tz au ps@mit.go.tz.   Unaombwa pia kutumia barua pepe tajwa endapo utaridhika na huduma zilizotolewa," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages