HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 23, 2019

TMA kununua rada tatu mpya

NA SULEIMAN MSUYA
KATIKA kuhakikisha huduma ya hali ya hewa nchini na nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) inakuwa na ubora, viwango na kuchochea ukuaji wa uchumi Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), inatarajia kununua rada tatu mpya za kisasa zitakazofungwa kwenye mikoa mitatu.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Huduma za Utabiri TMA, Dk. Hamza Kabelwa wakati akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki ambao mamlaka hiyo ilishiriki Mkutano wa Mawaziri wa Sekta ya Tehama, Habari, Uchukuzi na Hali ya Hewa kwa nchi za SADC ulifanyika jijini Dar es Salaam.
Dk.Kabelwa alisema TMA kwa sasa ina rada mbili za kisasa ambazo zimefungwa mkoani Dar es Salaam na Mwanza ambapo zinatumiwa kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa Tanzania na nchi za SADC.

Alisema rada nyingine tatu ambazo wanatarajia kununua hivi karibuni zitafungwa mkoa wa Mtwara, Mbeya na Kigoma hali ambayo itaongeza ufanisi wa utabiri kwa mamlaka hiyo na nchi jirani katika kukabiliana na majanga mbalimbali.
Mkurugemzi huyo alisema serikali ya Tanzania imedhamiria kuwa chanzo muhimu cha hali ya hewa kwa nchi za SADC hivyo haina budi kununua rada hizo za kisasa ikiwa ni pamoja na kutekeleza makubaliano ambayo nchi za jumuiya hiyo zimekubaliana.
"Mkutano huu ni muhimu kwa nchi za SADC, sekta ambayo tunaisimamia ya hali ya hewa ni moja ya mjadala ulichukua nafasi, hivyo tumeelezea mikakati yetu katika eneo hilo kwamba tunaendelea kufunga rada mpya za kisasa siku za karibuni hivyo nchi za SADC zitanufaika," alisema.
Dk.Kabelwa alisema iwapo nchi zote za SADC zitakuwa na rada za kisasa kama Mkataba wa Minamata unavyotaka ni dhahiri masuala ya utabiri wa hali ya hewa yatakuwa bora na nzuri.
Mkurugwnzi huyo alisema mkataba huo unataka kuachana na matumizi ya zebaki kwa kuwa ni chanzo cha uharibifu wa mazingira duniani hivyo Tanzania imeanza kutekeleza.
Alisema iwapo TMA itakuwa na miundombinu ya kisasa ya kufuatilia utabiri wa hali ya hewa ni wazi kuwa mamlaka hiyo itakuwa kichocheo cha ukuzaji uchumi kwa nchi za SADC na Tanzania.
"Taarifa zetu zinasaidia wakulima kwa kutoa taarifa za mvua za msimu,  wavuvi, wasafiri, wafanyabishara na serikali kwa ujumla kupanga mipango yake hivyo iwapo taarifa zinakuwa sahihi ni dhahiri kuwa madhara hayatakuwepo kwa jamii na kama yakitokea yanaweza kudhibitiwa," alisema.
Kabelwa alisema iwapo mifumo ya kupata taarifa za hali ya hewa sahihi itakuwepo ni dhahiri kuwa shughuli za uokoaji zitakuwa nzuri pia.

No comments:

Post a Comment

Pages