HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 27, 2019

UANDISHI VITABU KUWA KIGEZO WAKUFUNZI KUPANDA VYEO MLALE

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu pichani katikati akiongea na wafanyakazi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale kilichopo kata ya Magagula Wilaya Songea Mkoani Ruvuma mapema jana mara baada ya kutembelea miradi inayoendelea chuoni hapo.


Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu ameagiza uongozi na wakufunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale kilichopo Kata ya Magugula  Wilaya Songea Mkoani Ruvuma kuanza kutumia kutumia vitabu kwa njia ya mtandao ili kuweza kutoa  taaluma inayoendana na wakati.
Dkt. Jingu amesema hayo wakati wa ziara yake chuoni hapo kwa lengo la kujiona maendeleo ya Chuo hicho lakini pia kusikiliza wafanyakazi ili kuangalia namna bora ya utendaji kazi kati ya Wizara yake na Chuo hicho ambayo inasimamia Vyuo vya Maendeleo ya Jamii.
Dkt. Jingu pamoja na kuwataka wakufunzi hao kutumia elimu ya mtandao kuboresha taaluma zao lakini pia amewataka wakufunzi hao kuanza kutumia Maktaba ya Kimtandao ili waweze kupata vitabu mbalimbali vilivyoandikwa kuhusiana na taaluma ya Maendeleo ya Jamii.
Dkt. Jingu pia amewataka wakufunzi Chuoni hapo kuanza kuandika vitabu ili kuweza kutoa taaluma inayoendana na wakati akionya kuwa inabidi upandaji vyeo wa wakufunzi ubadilishwe ili uandishi wa vitabu uwe moja ya kigezo muhimu cha kupandisha vyeo kwa wakufunzi wanaofundisha taaluma ya Maendeleo ya Jamii.
‘’Mnaona mnatoa welimu sahihi kumbe mnatumia elimu ya miaka 47 iliyopita hivyo nawataka muandike vitabu kwa lengo la kutoa elimu inayoendana na wakati ingawa najua kuwa pamoja na uandishi wa vitabu hivyo haviwezi kutosha ila kwasasa mnaweza  kutumia Maktaba ya Mtandao itakayowaezesha kupata vitabu kutoka vyanzo mbalimbali mtandaoni.’’ Alisisitiza Dkt. Jingu
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale Bi. Luciana Mvula amezitaja changamoto zinazokabili chuo hicho kuwa ni pamoja na upungufu wa vyumba  vya madarasa chuoni hapo lakini pia upungufu wa vitendea kazi kama compyuta na gari kwa ajili ya huduma za dharula kama vile ugonjwa kwa wanafunzi na watumishi wa chuo hicho.
Bi .Mvula pia imeitaja changamoto ya upungufu vitabu katika Maktaba ya Chuo hicho na kumuomba Katibu Mkuu Wizara ya Afya kuangalia namna bora ya kuwezesha chuo kuboresha Maktaba hiyo lakini pia kukarabati majengo ya zamani ya chuo hicho ambayo imeanza kuchakaa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu anaendelea na Ziara ya Siku Tano katika Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kutembelea vyuo vya Maendeleo ya Jamii na pia Makazi ya Wazee yaliyoko katika Mikoa hiyo.

No comments:

Post a Comment

Pages