HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 17, 2019

Wamiliki wa Hospitali, Zahanati binafsi kukopeshwa mabilioni

 Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia) na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati, wakizindua huduma ya Afya Loan uliofanyika jijini Dar es Salaam. 
Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi (wa pili kulia), akipeana mikono na Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati, baada ya kuzindua huduma ya Afya Loan uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa na wa Kati wa benki hiyo, Donatus Richard, Mwenyekiti wa Bodi ya Hospitali ya Heameda, Edwina Lupembe (kushoto) na Mkurugenzi Mkazi wa Medical Credit Fund, Dk. Heri Marwa. (Na Mpiga Picha Wetu). 
 Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB, Filbert Mponzi, akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa huduma ya Afya Loan uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa hafla ya uzinduzi wa huduma ya Afya Loan ya Benki ya NMB.

Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Elisha Osati, akizungumza wakati wa uzinduzi huduma ya Afya Loan.


NA MWANDISHI WETU

KATIKA kutanua wigo wa wadau wa Sekta ya Afya nchini kukabiliana na changamoto zinazoikabili nyanja hiyo, Benki ya NMB kwa kushirikia na Shirika la Medical Credit Fund (MCF), imezindua huduma maalum ya mikopo nafuu kwa wamiliki wa hospitali binafsi, vituo vya afya na zahanati.

Uzinduzi wa huduma hiyo ya ‘NMB Afya Loan,’ umefanyika jana katika Hospitali ya Heameda Medical Clinic, iliyopo Bunju B jijini Dar es Salaam, ambapo NMB itatoa mikopo kuanzia Sh. Milioni 2 hadi Sh. Bil. 5, wakati MCF inatoa dhamana ya asilimia 50 katika mikopo yote.

Kwa mujibu wa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Filbert Mponzi, wanufaika wakuu wa Mkopo wa Afya ni hospitali binafsi, vituo vya afya na zahanati, maduka ya dawa na wasambazaji wa dawa ili kuwezesha, kuiinua na kuboresha biashara za huduma za afya nchini.

Mponzi alibainisha kuwa, ushirikiano baina ya NMB na MCF (aliowataja kama wabobevu wa Sekta ya Afya), unaihakikishia jamii ya Watanzania huduma bora za afya kutoka katika vituo, zahanati na hospitali zote zitakazoamua kufanya aina hiyo ya uwekezaji.

Aliongeza kuwa hadi uzinduzi unapofanyika, zaidi ya vituo vya afya, zahanati na hospitali 200 zimeshachukua Mikopo ya Afya, huku akiwataka wadau walioamua kuwekeza katika sekta ya afya, kuchangamkia Afya Loan ili kujenga misingi ya huduma bora za kitabibu.

"Kuna fursa nyingi katika Sekta ya Afya nchini na sisi kama NMB, tumeliona hili na tumejikita kuwapa nafasi hospitali, vituo vya afya wasambazaji wa vifaa tiba kujiendeleza.  Tuna imani huduma hii itachangia kwa kiasi kikubwa utoaji wa huduma kwa afya za bei nafuu," alisema Mponzi.

Naye Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania (MAT), Elisha Osati ambaye alikuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo, aliwataka madaktari na wadau wa sekta hiyo kuchangamkia Huduma ya Afya Loan, ili kutanua wigo wa ajira ili kukabiliana na ongezeko la madaktari wapya katika soko la ajira.

Osati alisema kumekuwa na madaktari wengi wapya wanaotokea vyuoni, ambao wanapata wakati mgumu katika soko la ajira na kwamba Afya Loan inaenda kuwapa fursa ya kuajiriwa na wadau watakaotumia mikopo hiyo kuanzisha hospitali, zahanati na vituo vya afya.

Aliitaka NMB kufanya mazingatio makubwa katika riba ya mikopo hiyo, ili kutoa nafasi kwa wadau wengi kujitokeza kukopa na kuboresha sekta ya afya na kujenga Tanzania yenye jamii inayomudu kukabiliana na changamoto za afya kwa maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa MCF, Dk. Heri Marwa, alisema Afya Loan imeboresha Sekta ya Afya katika nchi za Afrika zinazohudumiwa na shirika hilo lenye Makao Makuu nchini Uholanzi, akizitaja kuwa ni Liberia, Nigeria, Ghana, Kenya, Uganda na sasa Tanzania.

Alisema MCF ni shirika linalojiendesha kwa kutotegemea faida, bali kujali afya na ustawi wa jamii na kwamba hiyo ndio siri ya kutoa dhamana ya asilimia 50 ya mikopo yote itakayotolewa na NMB kupitia Afya Loan, ili kwenda kupunguza kama sio kumaliza changamoto za kitiba.

"Upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya uwekezaji ni changamoto kubwa katika nchi nyingi za Kiafrika na inazuia utoaji huduma nafuu. Kwa huduma hii tunafurahi kwamba hospitali nyingi binafsi, vituo vya afya vitapata na uwezo wa kuwekeza kwenye vifaa vya afya vya kisasa,” alisema Dk. Marwa.

No comments:

Post a Comment

Pages