HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

September 04, 2019

Wanakijiji waomba msaada nyumba ya mganga

 Muuguzi wa zahanati ya kijiji cha Ughaugha, Elisha Makalla akizingumzia changamoto za utoaji huduma kwenye zahanati hiyo iliyojengwa na TASAF kwa kushirikiana na wanakijiji.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ughaugha A, Iddi Labia, akiwaonesha baadhi ya waandishi wa habari sehemu ya eneo la zahanati hiyo itakapojengwa nyumba ya mganga.

NA MWANDISHI WETU, SINGIDA

WAKAZI wa Kijiji cha Ughaugha A wameiomba serikali kuwajengea nyumba ya mganga na watumishi wa Zahanati ya kijiji hicho iliyojengwa kwa nguvu za wananchi chini ya Mpango wa Kunusuru Kaya maskini zaidi hapa nchini (TASAF).

Wakizungumza kwenye viwanja vya zahanati hiyo juzi walipotembelewa na baadhi ya maofisa wa TASAF, wananchi hao walishukuru kwa kusogezewa huduma za afya huku wakiomba ubora wa huduma hizo na upatikanaji wake kwa saa24.

Benedicto Agustino mkazi wa kijiji hicho alisema licha ya kuwepo kwa zahanati hiyo huduma zinapatikana kwa saa 12 kwa kuwa wahudumu wanalazimika kurudi mjini.
"TASAF wamesaidia sana maana tulikuwa tunakwenda zaidi ya kilometa nane kufuata Kituo cha afya Makiungu hali ilikuwa mbaya zaidi wakati wa mvua njia hazipitiki wagonjwa tunawabeba kwenye machela.

"Sasa hapa Ughaugha tumepata zahanati lakini haisaidii yaani lengo halijafikiwa. Mtu akiugua kuanzia saa1 usiku anaweza kufa kwa kukosa matibabu," alisema Agustino.

Amina Hema ni miongoni mwa wakazi wa Ughaugha anayeiomba serikali kuharakisha nyumba za watumishi wa zahanati ili azma ya uwepo wa huduma za afya karibu na wananchi lifikiwe kwa kuwa imepunguza gharama za usafiri kwenda Makiungu na mgonjwa kufuata matibabu.

"Tumeshuhudia wajawazito wanazalia njiani na hivi karibuni kilitokea kifo mama alifariki mtoto alibaki mpaka leo yupo sasa hii hatutaki iendelee zahanati ipo tupate huduma muda wote," alisema Hema.

Akizungumzia ujenzi wa zahanati ya Ughaugha, Mwenyekiti wa mradi wa zahanati hiyo, Fadhili Mdachi alisema wananchi waliomba kupata huduma za afya karibu wakati wa mkutano kati yao na watendaji wa TASAF.

"Baada ya wananchi kuibua kero ya kukosa zahanati TASAF walitoa fedha Ujenzi ukaanza Oktoba 2015 ukakamilika Juni 2016 kabla ya kuanza kazi rasmi Mei 2019.

"Gharama za ujenzi wa zahanati hii ni Sh milioni 66 na nguvu za wananchi ambao tulishirikiana sana katika kukamilisha ujenzi," alisisitiza Mdachi.

Ofisa Mtendaji wa kijiji cha Ughaugha kwenye Kata ya Unyamikumbi Manispaa ya Singida, Iddi Labia alisema suala la nyumba za watumishi wa zahanati hiyo linafanyiwa kazi kwa kuwaruhusuu  kutumia nyumba za walimu ambazo kwa sasa hazitumiki.

"Hilo ni tatizo tunalijua tulishaliongea na diwani na mbunge pia hao viongozi hadi mwisho wa Septemba tutapata umeme na watumishi hawa wawili wataanza kuishi kwenye nyumba za walimu," alisema.

Muuguzi Elisha Makalla aliyezungumza kwa niaba ya Mganga Mkuu wa zahanati hiyo, alisema walianza kazi Mei13 mwaka huu na kutibu wagonjwa 600 kwa mwezi mmoja.

"Mahitaji ya huduma hapa ni makubwa changamoto iliyopo ni makazi, idadi ya watumishi na vifaatiba... tupo watumishi wawili na wote tunaishi mjini inanilazimu kutumia Sh. 6000 kwenda na kurudi nyumbani kuanzia jumatatu hadi ijumaa," alisema muuguzi huyo.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ughaugha A, Iddi Labia akiwaonesha baadhi ya waandishi wa habari sehemu ya eneo la zahanati hiyo itakapojengwa nyumba ya mganga.

No comments:

Post a Comment

Pages