*Amwagiza Mkuu wa Mkoa aungalie vizuri mkoa wake
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemsimamisha kazi Mhandisi wa Ujenzi wa wilaya ya
Morogoro, Brown Undule baada ya kushindwa kutekeleza majukumu yake
ipasavyo, ikiwemo usimamizi mbovu wa ujenzi wa kituo cha afya Mkuyuni.
Amemsimamisha
kazi Mhandisi huyo leo (Jumatano, Septemba 18, 2019) baada ya kukagua
ujenzi wa kituo hicho cha afya akiwa katika siku ya tano ya ziara yake
ya kikazi mkoani Morogoro. Amesema hajaridhishwa na aina ya milango
iliyotumika.
“Milango
yote katika jengo hili ing’olewe leo leo, huwezi kuweka milango ya
hovyo namna hii yaani mtu wa nje anamuona aliyeko ndani, nimesitisha
kuendelea kukagua jengo. Yeye na usomi wake ameridhishwa na milango ya
hovyo kama hii.”
Waziri
Mkuu amesema aina ya milango iliyowekwa katika kituo hicho cha afya
haiwezi kutumika hata kwenye nyumba ya mtu binafsi, lakini kutokana na
uangalizi mbovu kutoka kwa watendaji walikubali kuweka milango hiyo
mibovu.
Amesema
Serikali imeamua kujenga vituo vya afya vitano kwenye wilaya hiyo ili
kusogeza huduma za afya kwa wananchi na kuwapunguzia kutembea umbali
mrefu kufuata huduma za afya, hivyo amewataka watendaji wasimamie
ipasavyo miradi hiyo.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Baada
ya kukagua ujenzi wa kituo hicho cha afya, Waziri Mkuu amekagua ujenzi
wa hospitali ya wilaya, ambako nako ameagiza kuong’olewa kwa mbao zote
zilizotumika kwa ajili ya kupaulia jengo la mama na mtoto la hospitali
hiyo kwa kuwa hazina viwango. “Fundi usiendelee na kazi hii ya upauaji
kwa sababu mbao unazotumia hazikidhi viwango.”
Kwa upande wake,
fundi anayejenga jengo hilo la mama na mtoto, Johnson Ishengoma amesema
changamoto kubwa anayoipata katika ujenzi huo ni ucheleweshwaji wa
vifaa pamoja na kulazimishwa kutumia vifaa vilivyo chini ya kiwango.
Fundi
huyo ametolea mfano suala la mbao za kupaulia kuwa aliomba mbao za
urefu wa futi 20 lakini aliletewa mbao zenye urefu wa futi 12 na
kulazimishwa azitumie hivyo hivyo. “Mhandisi wa wilaya Brown Undule na
mtu wa manunuzi Grace ndio wanaoniletea vifaa hivi. Baadhi ya vifaa huwa
navikataa kutokana na kutokuwa na ubora.”
Katika hatua nyingine,Waziri
Mkuu amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dkt. Steven Kebwe kuuangalia
vizuri mkoa wake na kuhakikisha anauchunga vizuri kwa sababu umekithiri
kwa matumizi mabaya ya fedha za umma.
“Wakati
nikiendelea na ziara mkoani hapa, nimepata taarifa kwamba zaidi ya
sh.milioni tisa zimetumika kwa ajili ya kilipana posho katika
Halmashauri ya mji Ifakara . Posho hizo ni kwa ajili ya ziara ya Waziri
Mkuu na imetoka kwa mtendaji wa kata ya Viwanja 60, hili jambo
halikubaliki. Nakukabidhi risiti zote na uwachukulie hatua wote
waliohusika. Mkoa wa Morogoro ni shida”
Wakingumzia
kuhusu utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano na ujenzi wa miradi ya
maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao, wakazi wa Tarafa ya Mkuyuni
wameipongeza Serikali kwa namna inavyowajali wananchi wake ikiwa ni
pamoja na kuboresha huduma.
Mmoja
wa wananchi hao, Uwesu Mwichumu (71) mkazi wa kijiji cha
Kibungo ameipongeza Serikali kwa usimamizi wa miradi na hatua
inazochukua kwa baadhi ya watendaji wanaojihusisha na wizi wa fedha za
umma.
Amesema
Serikali inajitahidi kuwaletea miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao
tatizo lililopo ni kwa watendaji wa chini. “Watendaji wengi huku chini
wanashindwa kutekeleza majuku yao ipasavyo, wanashirikiana na wazabuni
kuiibia Serikali.”
Mkazi
mwingine wa Tarafa hiyo, Hanifa Shaban amesema anaishukuru Serikali kwa
kuboresha huduma mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa dawa katika vituo
vya afya na zahanati. Amesema awali walikuwa wanakwenda zahanati na
kuandikiwa vyeti bila ya kupewa dawa , hivyo walilazimika kwenda kununua
kwenye maduka ya dawa jambo ambalo kwa sasa halipo.
No comments:
Post a Comment