Mthamini Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha akiangalia moja ya nyumba iliyofanyiwa uthamini kwa ajili ya kulipwa fidia katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara kupisha upanuzi wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa ajili ya ujenzi wa bwawa la taka sumu jana. Kulia ni Mthamini kutoka wilaya ya Serengeti Bariki Ileta.
Na Munir Shemweta, WANMM NYAMONGO
Serikali imeanza
kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Nyamongo katika wilaya ya
Tarime mkoani Mara kwa kuanza kufanya tathmini ya fidia ya kutwaa eneo la ardhi
kwa ajili ya kupanua Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara ili kujenga Bwawa la
Maji Taka.
Tayari timu ya
wataalamu 25 kutoka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inayojumisha Ofisi
ya Mthamini Mkuu wa Serikali pamoja na idara ya Upimaji na Ramani iko eneo la
Nyamongo kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoani Mara kutathmini mali za wananchi
ili kulipwa fidia na kupata eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa la Maji Taka.
Akizungumza wakati wa
zoezi hilo jana katika kijiji cha Matongo wilaya ya Tarime mkoa wa Mara Mthamini
Mkuu wa Serikali Evaline Mugasha alisema, zoezi la uthamini linalofanyika ni kwa
ajili ya kutwaa eneo la ujenzi wa Bwawa la Maji Taka katika eneo la Nyamongo lenye
ukubwa wa hekta 237 ambalo linahusisha vitongoji vitatu vya Kigonga A,
Kwinyunywi na Kigonga B ambapo uthamini wake ulishaanza toka mwezi julai mwaka
huu.
Mugasha alisema,
uthamini huo unaangalia mali inayohamishika na ile isiyohamishika na kufuata
sheria ya ardhi na ile ya kijiji na kusisitiza uthamini huo umekuwa ukifanyika
kwa uwazi na hauna lengo la kumnufaisha au kumpunja mtu yeyote.
‘’ Eneo la Nyamongo tunalichukulia
kama eneo la mfano hasa baada ya kufanyika tathmni maeneo mbalimbali ya mgodi miaka
ya nyuma na kubaini udanganyifu wa baadhi ya wananchi na Wathamni wasiowaaminifu
kutumia zoezi kama hili kujinufaisha’’ alisema Mugasha.
Kwa mujibu wa Mthamini
Mkuu wa Serikali, udanganyifu wowote utakaofanyika kwa nia ya mmiliki wa nyumba
ama eneo kujinufaisha Ofisi yake haitamvumilia kwa kuwa baada ya uthamini wanafanya
uhakiki kujiridhisha usahihi wa taarifa na mali za wananchi.
Mthamini kutoka ofisi
ya Mkuu wa mkoa wa Simiyu Lazaro Mayumba anayeshiriki zoezi hilo alisema, zoezi
hilo linafanyika kwa kasi kwa kuwa serikali ina jukumu la kulinda mali na afya
za wananchi waliokuwa wakilalamikia kwa muda mrefu kuhusu kutiririka maji yenye
sumu katika Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara.
Alieleza kuwa, katika
kuhakikisha wananchi wanaozunguka mgodi huo hawaathiriki na wakati huo mgodi haufungwi
kutokana na madhara yanayopatikana dhidi ya taka sumu, serikali iliona iko haja
kutwaa eneo litakalosaidia mgodi kupata eneo kwa ajili ya ujenzi bwawa kubwa na
lenye ubora ambalo halitaleta madhara yanayodaiwa na wananchi.
''Mbali na madai ya wananchi
wanaozunguka mgodi wa North Mara lakini pia athari za taka sumu zinaweza kufika
mto Mara ambao uko umbali wa takriban kilometa tatu kutoka katika Mgodi na kama
hatua za haraka hazitachukuliwa unaweza kuharibu uoto wa asili pamoja na mbuga
za wanyama''' alisema Mayumba.
Baadhi ya wananchi wa
kijiji cha Matongo linakofanyika zoezi la Uthamini wameonesha kufurahishwa na
hatua ya serikali kuamua kutafuta eneo kwa ajili ya ujenzi wa Bwawa jipya la
taka sumu za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa madai kuwa wamekuwa
wakiathirika sana na maji yanayotiririka katika mgodi huo.
Gaga Sita Kishashila mmoja
wa wakazi wa kijiji cha Matonga alisema pamoja na zoezi la uthamini
linaloendelea sasa lakini shauku kubwa ya wakazi hao ni kutaka kujua wanalipwa
lini ili waweze kuondoka maeneo hayo mapema na hofu yao ni kukwama kwa zoezi
hilo kama ilivyotokea huko nyuma.
Mkazi
mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Simion Kirario aliomba uthamini
unaofanyika kuangalia na hali za wananchi hao kwa kuwa baadhi yao wana
hofu ya kulipwa kiasi kidogo kutokana na aina ya nyumba wanazomiliki za
Msonge huku wakihitaji kuwa na fedha nzuri itakayowawezesha kununua eneo
lingine na kufanya maendelezo.
Mwenyekiti wa Kitongoni
cha Kigonga A Kibwabwa Mwita Kibwabwa alisema kazi ya uthamni katika kitongoji
chake imeenda vizuri kwa kuwa zoezi hilo linafanyika kwa kasi na wananchi wake
wanataka kujua wanalipwa lini. Hata hivyo alisema baadhi ya wananchi
wamelalamikia kiasi watakacholipwa na kukiona kidogo ukilinganisha na matarajio
yao.
Kwa muda mrefu wananchi
wa Nyamongo wilaya ya Tarime mkoa wa mara hasa wale wanaoishi vitongoji
vinavozunguka Mgodi wa Dhahabu wa ACACIA North Mara wamekuwa wakilalamikia
uchafuzi wa mazingira hasa maji yanayovuja kutoka Mgodi huo kuwa yana sumu inayoathiri
afya zao jambo lililomlazimu Rais John Pombe Magufuli wakati wa ziara yake
katika eneo hilo kuagiza kufanyika utafiti ili kubaini ukweli huo.
No comments:
Post a Comment