Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa ameshika kipande cha tofali, kilichobomoka, wakati akikagua kituo cha afya cha Ndago, wilayani Iramba, katika Mkoa wa Singida, na kutoridhishwa na ujenzi wa kituo hicho, Oktoba 6.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na mtaalam wa maabara, Bahati Ipunda, wakati akikagua kituo cha afya cha Wilaya ya
Ikungi, mkoani Singida, Oktoba 6.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hajaridhishwa na ujenzi wa kituo cha afya cha Ndago, wilayani Iramba mkoani Singida kwa sababu uko chini ya kiwango.
Ametoa kauli
hiyo leo (Jumapili, Oktoba 6, 2019), wakati akizungumza na wananchi wa kata ya
Ndago mara baada ya kukagua majengo ya kituo hicho.
“Nimepita
kote nchini kukagua vituo hivi lakini hapa wamenikasirisha. Wamenileta kwenye
jengo nilikaguem nikajua ni jipya kumbe ni la zamani. Lazima nikiri kwamba
fedha yetu hapa haijakamilika, jengo la mama na mtoto halijakamilika.
Nilipouliza linakamilika lini, wananijibu tuko kwenye final touches (tuko hatua
za mwisho),” amesema.
“Jengo lile
halivutii kabisa, wanaotoa maelezo hakuna kinachoeleweka. Sijaridhishwa kabisa
na hali hii. Jengo la upasuaji nalo pia nimeona ni la zamani. Hii ina maana
hamjajenga jengo jipya. Mimi nataka nione jengo jipya hapa,” amesisitiza.
Alipomuuliza
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Bw, Leno Mwageni amebakiza kiasi gani cha fedha
katika sh. milioni 400 ambazo zililetwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo hayo,
Mkurugenzi huyo alijibu kwamba hakuna kiasi cha fedha kilichobakia.
Waziri Mkuu
aliwaeleza wananchi hao kwamba Mheshimiwa Rais John Magufuli anatambua wao
hawana uwezo, na tena wanaugua na kuna watu ambao wanapoteza maisha kwa sababu
hawawezi kufika kwenye tiba kwa wakati.
“Vituo vya afya
vinajengwa kila mahali nchini ili wewe mwananchi usilipe nauli kwenda Iramba
mjini au Singida mjini kutafuta tiba, bali upate vipimo vyote hapa hapa ulipo.
Vipimo vya magonjwa yote vinapatikana hapa hapa.”
“Fedha hizi
zikiletwa zinataka pajengwe maabara, chumba cha upasuaji mdogo na mkubwa,
chumba cha huduma ya mama na mtoto, chumba cha kuhifadhia maiti na nyumba ya
mkuu wa kituo, lakini hapa Ndago fedha yetu imeharibika,” amesema.
Alipoenda
kukagua chumba cha kuhifadhia maiti, Waziri Mkuu alikuta limewekwa mlango wa
mbele tu na vyumba vingine vyote havina milango wala mabomba na masinki hayajakamilika
tofauti na taarifa aliyopewa kwamba jengo hilo liko tayari.
“Mkurugenzi
nimekuta wagonjwa wamelazwa katika baadhi ya vyumba na kazi haijakamilika.
Huwezi kupanga vifaa wakati ujenzi unaoendelea ili kumdanganya Waziri Mkuu. Na
wala hunidanganyi mimi bali unawadanganya wananchi.”
“Ninazo
taarifa kwamba jana mlikesha kupanga vitu ndani. Nenda kaondoe vifaa vyote hadi
ujenzi utakapokamilika ndipo madaktari warudi kuendelea na kazi. Serikali hii
haiwezi kuvumilia vitu vya hovyo. Hatua kali zitachukuliwa,” alisisitiza.
Mapema, Mbunge wa jimbo hilo, Bw. Mwigulu
Nchemba alimweleza Waziri Mkuu kwamba alichangia mifuko 400 ya saruji na
wananchi wa kata hiyo walichangia mawe na ujenzi wa msingi.
Alitumia
fursa hiyo kumshukuru Rais Magufuli kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa vituo vya
afya. “Tunashukuru kwa sababu fedha hizi zimekuja kamili, na siyo kwa mafungu.
Wananchi wamechangia nguvu zao na mimi mwenyewe nilitoa mifuko 400 ya saruji,”
alisema.
Alitumia
fursa hiyo kumuomba Waziri Mkuu awasaidie wananchi wa kata ya Ndago wapate
barabara ya lami ya kutoka Singida-Sepuka-Ndago-Kizaga yenye urefu wa kilometa
76. “Hii ni tarafa kubwa kuliko zote na huku ndiko uzalishaji mkubwa uliko. Hii
barabara imeshafanyiwa upembuzi yakinifu, kilio na furaha ya wana-Ndago ni
barabara hii kuwekwa lami,” alisema.
No comments:
Post a Comment