Mkandarasi
anayetekeleza mradi wa umeme vijijini katika wilaya za Buhigwe, Uvinza, Kasulu
na Kigoma Vijijini, mkoani Kigoma, Kampuni ya CCCE Etern Consortium,
akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wake kwa Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Oktoba 4, 2019.
Na Veronica Simba – Kigoma
Mmoja wa wakandarasi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini mkoani Kigoma; Kampuni ya Urban and Rural Engineering Services Ltd, huenda akapoteza sifa ya kupewa kazi nyingine ya aina hiyo na serikali, endapo hatarekebisha udhaifu aliouonesha kwa kufanya kazi kwa kusuasua.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 4, 2019 na Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya Bodi ya Wakurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Styden Rwebangila, baada ya kufanya ziara kukagua miradi ya umeme vijijini inayotekelezwa mkoani humo pamoja na kufanya kikao na wakandarasi husika; akiwa amefuatana na Mjumbe mwingine wa Bodi, Louis Accaro, wataalam wa Wakala huo pamoja na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya ziara hiyo, Mhandisi Rwebangira alisema kwamba Bodi imejiridhisha na utendaji kazi wa Mkandarasi kutoka China, Kampuni ya CCCE Etern Consortium lakini akasema wamebaini matatizo makubwa upande wa kampuni ya kizalendo ya Urban and Rural Emgineering Services Ltd.
Akieleza zaidi, alisema mkandarasi husika ameonesha uzembe mkubwa wa kazi katika maeneo anakotekeleza mradi ambayo ni Kibondo na Kakonkwo kwani amefikia asilimia 34 tu kati ya 62 aliyopaswa kuwa ameifikia hadi sasa.
“Aidha, tangu mwaka huu uanze, amejenga kilomita 3.8 tu ya njia ya umeme wa msongo wa kati, kutoka kilomita 220 alizokuwa amebakiza.
Kwahiyo, ametupa wasiwasi kuwa ataweza kukamilisha kazi kwa wakati kama ilivyo katika makubaliano na maelekezo ya serikali,” alieleza Mwenyekiti.
Akifafanua zaidi, Mhandisi Rwebangila alisema hata utetezi alioutoa mkandarasi huyo wakati akihojiwa na Bodi husika hauna mashiko kwani changamoto alizodai zinamkabili ikiwemo ya ucheleweshwaji wa malipo, tayari serikali ilikwishazifanyia kazi na kuzitatua.
“Kwa sababu ametelekeza kazi na hajaagiza vifaa kwa muda mrefu, hata hajui ni mabadiliko gani yamefanyika.”
Aliongeza kuwa, Bodi hiyo imefadhaishwa zaidi na kitendo cha mkandarasi anayehusika ambaye ni mkurugenzi wa kampuni kutokuja mwenyewe kukutana nao na badala yake akamtuma mwakilishi ambaye ni msimamizi
wa miradi.
Alisema, kwa sababu hiyo, Bodi imetoa maagizo kwake kuwa ahakikishe anafika mwenyewe kukutana nayo, itakapokuwa mkoani Kilimanjaro ambako nako anatekeleza mradi husika pia.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Accaro, aliongezea kwamba kutokana na utendaji usioridhisha wa mkandarasi huyo, Bodi imepoteza matumaini kuwa anafaa kuendelea na kazi husika, lakini akasema maamuzi rasmi yatafanywa baada ya kukamilisha ziara husika katika mikoa iliyosalia na kuwasilisha ripoti kwa Bodi nzima ya REA, kwakuwa wao wanawawakilisha wenzao katika ziara hiyo.
Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti, mkandarasi kutoka China alisema ataendelea kufanya kazi kwa bidii ili kukamilisha kazi yake kwa wakati kama ilivyoelekezwa na serikali ilhali mkandarasi mzawa alisema atajitahidi kufanyia kazi maelekezo aliyopewa na Bodi ili kurekebisha udhaifu ulioonekana.
Katika hatua nyingine, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi kutoka REA, ambaye amefuatana na Bodi katika ziara hiyo, aliwataka wananchi kutokuwa na hofu kwamba miradi ya REA inapokamilika na kukabidhiwa kwa TANESCO, watalipishwa gharama zaidi.
Alisema, pamoja na miradi hiyo kukabidhiwa kwa TANESCO
itakapokamilika, wananchi wataendelea kutozwa gharama ileile ya shilingi 27,000 kama ilivyoelekezwa na serikali kwa miradi yote ya umeme vijijini.
Kamati hiyo ya Ufundi ya Bodi ya REA inaendelea na ziara yake katika mikoa mbalimbali nchini, ikiiwakilisha Bodi nzima katika kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme vijijini, hususan katika maeneo ambako
miradi hiyo inasuasua.
No comments:
Post a Comment