Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),
Wilhelm Gidabuday, akimkabidhi baadhi ya nyaraka Kaimu Katibu
Mkuu, Ombeni Zavala (kushoto), wakati wa makabidhiano yaliyofanyika jijini
Dar es Salaam, juzi. Wanaoshuhudia kutoka kulia ni Aziza Pembe, John Steven (wahudumu),
na Rahel Swai (Katibu Muhtasi).
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
ALIYEKUWA Katibu Mkuu wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT),
Wilhelm Gidabuday, amekabidhi rasmi ofisi ya shirikisho hilo baada ya kujiuzulu
hivi karibuni.
Gidabuday, alijiuzulu wadhifa huo kwa maslahi mapana ya RT
Novemba Mosi, katika kikao cha Kamati Tendaji kilichofanyika jijini Dar es
Salaam, ambacho kiliridhia uamuzi huo.
Makabidhiano hayo yalifanyika juzi katika ofisi za Shirikisho
hilo, Temeke jijini Dar es Salaam, mbele ya Kaimu Katibu Mkuu, Ombeni Zavala,
Makamu wa Kwanza wa Rais Utawala na Fedha, William Kallaghe na wafanyakazi wa
shirikisho hilo.
Makabidhiano yalihusisha nyaraka mbalimbali, vifaa na madeni
huku baadhi ya nyaraka chache zilizosalia Katibu huyo aliyejiuzulu akiahidi kumalizia
kuzikabidhi ndani ya wiki moja.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Gidabuday alisema
anashukuru anaondoka RT salama na kuahidi kuendelea kuwa mwanafamilia mwema wa
Riadha.
“Nashukuru Wajumbe wa Kamati Tendaji kwa kunikubalia
kujiuzulu kwangu kwa moyo mmoja, hivi sasa nitakuwa na muda wa kutosha na niko
tayari kutoa mchango wangu pale nitakapohitajika,” alisema Gidabuday na
kuongeza hivi sasa atakuwa anapatikana mkoani Arusha na Manyara
akijishughulisha na kuandaa maandiko mbalimbali ya miradi ya michezo na kukuza
vipaji hususan mkoani Manyara.
Naye Kaimu Katibu Mkuu, Zavala, aliwaondoa hofu wanafamilia
ya Riadha hususan wachezaji kuwa wasisite kumuona pale watakapokuwa wakihitaji
msaada.
Zavala, aliwaomba wajumbe wa Kamati Tendaji, kumpa
ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu ya shirikisho hilo.
RT inatarajiwa kufanya mkutano wake mkuu Desemba mwaka huu,
ambako katika moja ya ajenda itakuwa mabadiliko ya Katiba, ikiwamo kuwa
Mtendaji Mkuu (CEO), badala ya katibu wa kuchaguliwa.
No comments:
Post a Comment