Mwanasheria wa Shirika la Kimataifa lisilo la Kibiashara linalojishughulisha na masuala ya ardhi la Landesa, Godfrey Massay akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), wakati wa mafunzo ya siku mbili kuhusu kampeni ya 'Linda ardhi ya mwanamke' yenye lengo la kuwasaidia wanawake kumiliki ardhi.
Na Janeth Jovin, Morogoro
SHIRIKA la Kimataifa lisilo la kibiashara linalojishughulisha na masuala ya ardhi la Landesa limesema kuwa , licha ya kuwepo kwa sheria na Sera zinazomtaka mwanamke kumiliki ardhi, bado jambo hilo limekuwa tatizo na halitekelezeki kwa kiwango kile kinachotakiwa hapa nchini.
Kutokana na changamoto hiyo, Shirika hilo limeamua kuja na kampeni ijulikanayo 'Linda ardhi ya Mwanamke' yenye lengo la kuziba mwaya uliopo kati ya Sera hizo na utekelezaji wa sheria ili kuweza kuwasaidia wanawake waweze kumiliki ardhi.
Akizungumza mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari kuhusiana na kampeni hiyo, Mmoja wa Wakurugenzi wa Bodi ya Landesa Edda Sanga anasema nchi imekuwa na mipango ya ardhi na Sera nzuri lakini zimekuwa hazitekeleki.
Anasema kuna haja ya kuhakikisha sheria na Sera zinatekelezeka kwakuwa wanawake wengi ndio wanashiriki kikamilifu katika kilimo hivyo wasipopata nafasi ya kumiliki ardhi yale yanayosema kwamba wanayaweza hawataweza kuyafanya.
"Kampeni hii si rahisi kama tunavyofikiria bali ni ngumu kwani bado jamii yetu nyingi haioni umuhimu wa mwanamke kumiliki ardhi, ili tuweze kufanikiwa waandishi wa habari mnapaswa kuwa wabunifu katika uandikaji wa stori zenu ambazo ndizo zinaweza kuifungua jamii na kuondokana na dhana potovu waliyonayo kwa wanawake," anasema.
Naye Mwanasheria wa Landesa, Godfrey Massay anasema ni muhimu mwanamke akamiliki ardhi kwani jambo hilo litamuwezesha kupata mikopo mbalimbali na kujikwamua kiuchumi.
"Watanzania wake kwa waume wanahaki ya kumiliki ardhi ila tunataka wanawake wapewe fursa ya kumiliki ardhi hiyo ili iwaletee maendeleo chanya katika familia zao kwa kuwaongezea kipato na hili linawezekana,"anasema Massay.
Aliongeza kuwa ili kuhakikisha kuwa wanawake wanamiliki ardhi kihalali bila kubughudhiwa ni lazima umiliki uwe wa kisheria kwani jambo.hilo litamuepusha kuweza kudhurumiwa na kuwa rahisi kwake kwenda mahakamani kuidai na kuipata hati na umiliki wake kwa kuwa unatambuliwa kisheria.
Massay alizitaja baadhi ya changamoto ambazo ni vikwazo kwa wanawake kumiliki ardhi ni pamoja na masuala ya mila na kutokujua sheria .
Naye mchambuzi wa masuala ya Ardhi kutoka Landesa, Khadija Mrisho anasema ni lazima kuwepo na mkakati wa kufanya kazi ya kuondoa mila na desturi zinazomzuia mwanamke kutambulika katika umiliki wa ardhi.
Khadija anasema pia kuna umuhimu wa kuongeza idadi ya ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi katika utekelezaji ambapo sehemu nyingi ushiriki wao unakua mdogo.
Katika hatua nyingine Khadija anasema Novemba 21, mwaka huu kutakuwa na ufunguzi wa kampeni hiyo ya Linda haki za mwanamke katika kumiliki ardhi, ambapo mgeni rasmi atakua Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Jinsia Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu atakua mgeni rasmi katika ufunguzi huo.
No comments:
Post a Comment