Na Suleiman Msuya
TAASISI isiyo ya
Kiserikali ya Tanzania Feminist & Youth Change (TAFEYOCO), imetoa
mapendekezo manne ya kuiwezesha jamii kushiriki uchaguzi; iwe kupiga au kupigiwa
kura katika chaguzi zinazofanyika nchini mara kwa mara.
TAFEYOCO inakuja na
mapendekezo hayo huku vyama vya siasa hasa vya upinzani vikilamikia mchakato wa
uchaguzi wa Serikali Mitaa kuwa uligubikwa na figisu nyingi hali ambayo
ilipelekea vyama nane kutangaza kujitoa.
Vyama ambavyo vilijitoa
kushiriki uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24 mwaka huu ni pamoja na Chadema,
ACT-Wazalendo, CUF, UPDP, CCK, NCCR-Mageuzi, NLD na vingine.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa
TAFEYOCO, Elvice Makumbo alitoa mapendekezo hayo ili iwe suluhu ya chaguzi zingine zitakazofanyika kwa siku za
usoni ikiwemo uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Alisema katika uchaguzi
huo wa Serikali za Mitaa, wamegundua changamoto nyingi kuanzia kwa wagombea,
wasimamizi na vyama vya siasa, hivyo wameona waje na mapendekezo yanayoweza
kusaidia chaguzi zijazo ziwe rahisi.
Makumbo alisema taasisi
yao inashauri Serikali ijikite katika utoaji wa elimu ya uraia ili wananchi
wawe na ufahamu kuhusu masuala yote ya uchaguzi.
“Pendekezo la pili
tunaomba asasi za kiraia zitumie nafasi yake kwa kuelimisha jamii kabla ya
uchaguzi kufanyika na kushiriki katika uangalizi wa uchaguzi,” alisema.
Mkurugenzi huyo alisema
pendekezo la nne ni kuviomba vyama vya siasa kudumisha ushirikiano na
mawasiliano kuanzia ngazi ya mitaa ili kuepusha migogoro kwenye vyama.
“Katika mchakato huu wa
uchaguzi tumeona mapungufu mengi moja wapo ni vyama kukosa mawasiliano ya
kiofisi ngazi ya chini hivyo inachangia baadhi ya maamuzi kugawanya wanachama,”
alisema.
Alisema changamoto
nyingine ambayo ilitokea ni wagombea kujaza fomu kwa mazoea akitolea mfano eneo
la kuandika jina la chama wameandika kwa kifupi hali ambayo ni kinyume na
sheria.
Mkurugenzi huyo alisema
jamii imeonesha dhamira ya kushiriki siasa na chaguzi lakini kuna baadhi ya
wanasiasa wamekuwa wakitumia majukwaa ya siasa vibaya kwa kupotosha umma.
Aidha, Makumbo alitoa
rai kwa vyama vya siasa kuacha tabia ya kususia uchaguzi kwasababu ndio njia ya
kupata viongozi sahihi watakaosaidia kusukuma gurudumu la maendeleo.
Alisema TAFEYOCO
ilishiriki kuangalia mchakato wa uchaguzi katika mkoa wa Dar es Salaam na Pwani
ambapo katika maeneo yalifanya uchaguzi mwamko ulikuwa mzuri.
No comments:
Post a Comment