Waziri Mkuu Kassim Majaliwa
akizindua mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza katika
Uwanja wa Jamuhuri jijini Dodoma leo. Novemba 14/2019 . Wengine kutoka kulia,
Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dkt. Teguest Mengtsu, Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Waziri
mkuu mstaafu wa Tanzania, John Malecela na Mwenyekiti
wa Kamati ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
kuanzia tarehe 17 - 23 Novemba, 2019 litaanza zoezi la kampeni za
uchaguzi wa Serikali za Mitaa, hivyo ametoa onyo kwa yeyote
atakayevuruga zoezi hilo kuwa atachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
“Vikundi
vya ulinzi wa jadi au vya ulinzi binafsi au vya mashabiki wa vyama vya
siasa havitaruhusiwa kutumika kwenye maeneo ya mikutano ya kampeni au
maeneo ya uchaguzi.”
Waziri Mkuu ametoa onyo hilo leo (Alhamisi, Novemba 14, 2019)alipozindua
Wiki ya Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasioambukiza sambamba na Mpango
wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa Yasiyoambukiza
Waziri
Mkuu amesema kuwa vyombo vya Ulinzi na Usalama hususan Jeshi la Polisi,
Mgambo wenye sare na Maafisa wanaosimamia ulinzi vitatumika kuhakikisha
kunakuwepo na utulivu wakati wa kampeni na uchaguzi.
Kadhalika,Waziri
Mkuu ametumia fursa hiyo kuendelea kuwahimiza wananchi kujitokeza kwa
wingi siku ya kupiga kura na Serikali imejipanga vya kutosha kuhakikisha
zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi.
Wakati huo huo, Waziri
Mkuu amewataka wananchi kuchukua hatua stahiki za kujikinga na magonjwa
yasiyoambukiza ikiwa ni pamoja na kubadili tabia na mwenendo wao wa
ulaji wa vyakula kwa kuongeza ulaji wa mbogamboga, matunda.
Waziri
Mkuu amesema kila mtu ana wajibu wa kudhibiti matumizi ya vilevi kama
sigara na pombe; kuhamasisha jamii kushiriki mazoezi au shughuli za
nguvu; kuzingatia mlo unaofaa hasa kwa kuondoa au kupunguza chumvi,
sukari na mafuta. “Tujipange kukabiliana na madhara mengine yatokanayo
na uharibifu wa mazingira na tabianchi.”
Waziri
Mkuu amesema wananchi wanatakiwa wajenge utamaduni wa kufanya mazoezi
angalau dakika 30 mara tatu kwa wiki. “Katika eneo hili, niweke
msisitizo kwa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa
kuendeleza utaratibu wa mazoezi uliozinduliwa na Makamu wa Rais Mama
Samia Suluh Hassan.
“Tuendelee
kuhamasisha kuanzisha na kujiunga kwenye vikundi vya mazoezi ya pamoja
ambavyo husaidia sana kuleta hamasa ya kufanya mazoezi. Tutumie vikundi
vya joggingvilivyopo kwenye kata na mitaa au vijiji vyetu ili kupata mwendelezo wa jitihada zao.
Amesema
Halmashauri zote zihakikishe zinatenga na kuyaendeleza maeneo ya wazi
katika kila kata au mitaa ili pamoja na shughuli nyingine wananchi pia
watumie maeneo hayo kwa ajili ya kufanya mazoezi.
“Kwa
upande wa wanafunzi kuanzia sasa kabla ya kuingia darasani wawe
wanakimbia mchaka mchaka ili waweze kujiimarisha kiafya jambo ambalo
litawaepusha na magonjwa yasiyoambukiza.”
Amesema
magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa tishio kwenye jamii na ulimwenguni
kote, takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mwaka 2016 zinaonesha
kuwa magonjwa hayo yanachangia zaidi ya vifo milioni 41, sawa na
asilimia 71 ya vifo vyote milioni 57 vilivyotokea mwaka 2016.
“Taarifa
za mwaka 2013 za Shirika la Maendeleo Duniani (UNDP) zinaonesha kuwa,
pamoja na changamoto hizo za kiafya, magonjwa yasiyoambukiza yanaathiri
sana nyanja nyingine za maisha. Inakadiriwa kuwa katika kipindi cha
miaka 20, kuanzia mwaka 2013 gharama zitokanazo na magonjwa haya
zitafikia Dola za Marekani trilioni 47.”
Waziri
Mkuu amesema fedha hizo zingeweza kutumika kupunguza umaskini kwa watu
bilioni 2.5 kwa kipindi cha miaka 50. Kwa nchi za uchumi wa kati na
chini, magonjwa hayo yatagharimu mataifa hayo Dola za Marekani, trilioni
saba katika kipindi cha 2011 hadi 2025.
Amesema
gharama hizo zinatokana na kuongezeka kwa gharama za huduma za matibabu
na upotevu wa nguvukazi unaosababishwa na maradhi hayo, mfano,
makadirio yanaonesha kuwa gharama za huduma kwa magonjwa yasiyoambukiza
itafikia asilimia 75 ya mzigo wote wa bajeti ya afya. Ugonjwa wa
kisukari pekee utagharimu zaidi ya Dola za Marekani bilioni 465 sawa na
asilimia 11 ya bajeti yote ya afya duniani.
Awali,Waziri
wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu
alisema magonjwa yasiyoambukiza yanajumuisha magonjwa ambayo hayawezi
kusambazwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.
Aliyataja
magonjwa hayo kuwa ni pumu, shinikizo la juu la damu, kisukari,
saratani, siko seli, magonjwa ya akili, ajali, magonjwa mengi ya macho,
kinywa, masikio, pua na koo. “Magonjwa haya yamekuwa yakiongezeka
duniani kote na kuathiri nyanja zote za kimaisha.”
Waziri
Ummy alisema katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita Tanzania
ilishuhudia ongezeko la idadi ya watu waliopatiwa huduma za magonjwa
yasiyoambukiza kutoka wagonjwa milioni 3.4 kwaka 2016 hadi wagonjwa
milioni 4.2 mwaka 2018, ilkiwa ni sawa na ongezeko la asilimia 24.
Kwa upande wao,
wadau wa masuala ya afya wameipongeza Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuongeza kiwango cha
bajeti ya dawa kutoka sh. bilioni 31 hadi sh. bilioni 270.
No comments:
Post a Comment