Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
akisalimiana na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Dar es
salaam(UDSM), Jaji Mstaafu, Damian Lubuva , wakati alipotembelea Chuo
cha Uvuvi Kunduchi, jijini Dar es Salaam Novemba 28, 2019. (Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akifafanuliwa jambo na Mwanafunzi wa Shahada ya
Uzamivu, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Aulath Mustafa, wakati
akiangalia nyanya zilizopandwa katika kitalu nyumba, kwenye Chuo cha
Uvuvi Kunduchi, jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Waziri
Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Walimu pamoja na Wanafunzi wa Chuo
cha Uvuvi kilichopo Kunduchi, jijini Dar es Salaam, wakati
alipotembelea Chuo hicho, Novemba 28, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema Tanzania inahitaji kupata watendaji wa sekta ya uvuvi kuanzia
ngazi ya vitongoji kwani kuna vijiji vina mito, maziwa na baadhi vimepakana na bahari
na hivyo kutoa fursa za uvuvi.
“Nchi yetu inahitaji
kupata watendaji kuanzia ngazi ya vitongoji kwani vipo vijiji vyenye fursa za
uvuvi hivyo vinahitaji maofisa ugani ili waweze kufanya kazi vijijini na katika
vitongoji, lengo likiwa ni kuwasaidia wavuvi wadogowadogo wajue namna bora ya
kuvua na kuhifadhi samaki,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa kauli leo jioni (Alhamisi, Novemba 28, 2019), wakati akizungungumza na
wahadhiri na wanafunzi mara baada ya ziara yake ya kutembelea Kampasi ya
Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Amesema hivi
sasa Serikali inaandaa mazingira mazuri ya kuendesha sekta ya uvuvi kwa kupata
watalaamu wa ngazi mbalimbali watakaoisimamia sekta hiyo.
“Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Pombe Magufuli ambayo imejikita katika
ujenzi wa uchumi wa viwanda inasisitiza uwepo wa vyuo vya ngazi mbalimbali ili tuweze
kupata watalaamu wa kuendesha viwanda vinavyojengwa nchini,” amesema.
Amesema Serikali
inawatambua na inawahitaji sana wasomi wanaopata taaluma zao katika vyuo
mbalimbali hapa nchini ikiwemo kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha
Dar es salaam ambayo kwa sasa inatumika kwa ajili ya kutoa mafunzo
kwa vitendo ya shahada ya awali, kufundishia na kufanya utafiti kwa wanafunzi wa
Shahada ya Uzamili pamoja na wafanyakazi watafiti.
Waziri Mkuu
amesema angependa kuona watafiti na watalaam wanapewa fursa ya kuongoza na
kusimamia maeneo mbalimbali yanayohusiana na utafiti walioufanya ili kupata
matokeo sahihi na chanya ya utafiti wao.
Amesisitiza
kuwa Dkt. John Pombe Magufuli alitoa maelekezo thabiti ambayo amemkabidhi
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Bw. Luhaga Mpina ambaye ameyafanyia
kazi na yameleta mafanikio makubwa katika sekta ya uvuvi nchini.
“Hatua ya
kwanza ya kuboresha sekta ya uvuvi ilikuwa ni kuwaondoa watumishi wabovu na
wasio waamifu na nafasi zao kuwapa watumishi wazuri, wenye
taaluma ya uvuvi, waaminifu na wanaojali zaidi maslahi ya Taifa,
kazi ambayo imefanywa na Waziri na watendaji wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi,”
amesema.
Naye Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera,
Bunge, Ajira, Kazi ,Vijana na Wenye Ulemavu, Bibi Jenista Mhagama
amesema Serikali inaitegemea sana Kampasi ya Kunduchi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa
vile watalaam wanaopata taaluma zao katika kampasi hiyo wanahitajika sana
katika maendeleo ya uvuvi nchini.
Amesema Serikali
ya Awamu ya Tano imeamua kujenga uchumi wa viwanda ambavyo vitatumia malighafi
inayopatikana nchini ikizalishwa na Watanzania wenyewe na bidhaa zake
kuuzwa ndani na nje ya nchi ili kupata fedha za kigeni.
Naye Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina amewahakikishia Watanzania
kuwa hivi sasa idadi ya samaki na mapato ya Serikali yanayotokana na uvuvi
yameongezeka.
Amesema kabla
ya Serikali ya Awamu ya Tano kuanza kazi ya usimamizi wa na udhibiti
wa uvuvi nchini, mauzo ya bidhaa za uvuvi nje ya nchi yalikuwa ni sh.
bilioni 371 kwa mwaka na hivi sasa Serikali inajipatia sh. biloni
691 kwa mwaka.
No comments:
Post a Comment