HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

November 28, 2019

MADIWANI HALMASHAURI YA KINONDONI WAMPONGEZA MKURUGENZI ARON KAGURUMJULI UFAULU WA DARASA LA SABA

Diwani wa Kunduchi, Michael Urio, akizungumza katika kikao cha robo ya mwaka cha baraza la madiwani kilichofanyika jijini Dar es Salaam. (Na Mpiga Picha Wetu).
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Kazi Madulu wa kwanza kushoto na Naibu Meya George Manyama, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Kamati ya mipango miji ambaye ni Diwani wa Kata ya Mwananyamala Songoro Mnyonge akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo.
 
 
Na Mwandishi Wetu 
 
 Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni kwa pamoja limempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo , Aron Kagurumjuli kwa jitihada zake zakuwezesha kufanya vizuri katika matokeo ya darasa la saba.

Wakizungumza katika kikao cha robo ya mwaka cha baraza la madiwani lililofanyika leo, madiwani hao wameeleza kuwa Mkurugenzi kagurumjuli amekuwa na ushirikiano mzuri na watendaji wake na hivyo kufanikisha kufanya vizuri kwenye matokeo ya darasa la saba. 

Naibu Meya wa Halmashauri hiyo, George Manyama amesema kuwa kama halmashauri imejipanga kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliomaliza darasa la saba wanapata nafasi ya kusoma na kwamba hakuna atakaye kaa nyumbani.

Amefafanua kuwa ushindi huo uliopatikana ni dira inayoonyesha kuwa hata matokeo ya kidato cha nne yatakuwa mazuri na kwamba Halmashauri ya Kinondoni itaongoza.

“ Niseme tu haya ni matokeo mazuri kwetu, baraza limepitisha maadhimio ya kubadili shule ya msingi Kijitonyama kuwa Sekondari, huu ni mpango uliofanywa na wataalamu wa  Halmashauri yetu, lakini pia bado tunaendelea kufanya upembuzi yakinifu kuangalia shule nyingine ambazo tunaweza kuzigeuza kuwa Sekondari.

Diwani wa Kata ya Mwananyamala, Songoro Mnyonge amesema kuwa Halmashauri ya Kinondoni katika matokeo yake ya darasa la saba mwaka huu imeshika nafasi ya tatu kitaifa huku kimkoa ikishika nafasi ya kwanza.

Songoro amefafanua kuwa,matokeo hayo yanatokana na jitihada za Mkurugenzi Kagurumjuli kwani amekuwa akiwasimamia vyema watendaji wake sambamba na kutoa ushirikiano jambo ambalo limewezesha kupata matokeo hayo mazuri.

Amesema kuwa kama madiwani watashirikiana kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofaulu wanapata nafasi ya kuingia kidato cha kwanza kwakuwa shule zipo na kwamba hakuna mwanafunzi ambaye atakaa nyumbani kwakukosa nafasi.

“ Pamoja na pongezi hizi, ni wakati sasa wakuhakikisha kuwa wote wanakwenda kusoma , kama baraza leo hii tumeadhimia kuwa shule ya msingi Kijitonyama itabadilishwa na kuwa Sekondari, shule hii inavyumba 20 vya madarasa , hivyo wote watapata nafasi ya kusoma” amefafanua Chongolo.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Kunduchi Michale Urio , amesema kuwa suala la elimu bure lililotolewa na Rais Dk. John Magufuli, limewezesha kuwa na idadi kubwa ya watoto wanaosoma, hivyo Halmashauri itaendelea kuweka jitihada za kuhakikisha kuwa wanapata nafasi za kusoma.

No comments:

Post a Comment

Pages