Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Serengeti, Ester Matiko, akisisitiza jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi za Makao Makuu ya chama hicho Kanda, iliyopo Mjini Shinyanga. Matiko alizungumzia mikakati mbalimbali ya chama hicho, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge mwaka 2020. (Picha na Sitta Tumma).
Na Sitta Tumma, Shinyanga
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya
Serengeti, kimetangaza mkakati wa kuanza kuzunguka maeneo yote kufanya
siasa.
Kimesema Chadema kinaamini mwaka 2020 watashinda Urais na
kuongoza nchi, hivyo wataunda Serikali tatu ya Tanganyika, Zanzibar na
ya Shirikisho.
Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya
Serengeti, Ester Matiko, alipozungumza na waandishi wa habari mjini
hapa, leo.
Alionya vyombo vya dola, akisema Chadema haitakubali kuvurugiwa tena mikutano yao.
"Msajili wa Vyama vya Siasa hadi sasa hajawahi kupokea lalamiko lolote lile la sisi kuzuiwa kufanya mikutano.
"Yaani kama vile hajui kuwa mikutano ambayo ipo kikatiba na
kisheria imezuiwa. Safari hii hatukubali, hatukubali," Matiko alisema
mbele ya wanahabari.
"Tuataka vyombo vya usalama visivuruge. Viheshimu Katiba, Sheria na haki za binadamu," alisisitiza.
"Sera yetu ni kuwa na Serikali tatu. Ya Tanganyika, ya
Zanzibar na ya Shirikisho (Muungano). Kila eneo litashughulikia
maendeleo ya watu wake.
"Lakini, tutakuwa na mabunge kila kanda na bajeti zake.
Huku Tanzania Bara Chadema tuna kanda nane, Zanzibar mbili," Mwenyekiti
Matiko alisema.
Hata hivyo, alimuomba Rais Dk. John Magufuli, kuitangazia dunia kuufuta Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika mwaka huu.
Alisema uchaguzi huo unatakiwa upangwe kufanyika kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2020, iwapo Ikulu haikuingilia kuvurugwa kwake.
"Wasipofuta, Chadema tutatumia mawaziri kivuli wetu waliopo
kisheria, kuwasemea wananchi kwenye Serikali za Mitaa," alisema Matiko.
Kiongozi huyo wa Chadema Kanda ya Serengeti, alisema iwapo
Serikali inaamini imefanya vizuri miaka minne iliyopita, ingeacha
uchaguzi wa Mitaa ufanyike, ili wapate mrejesho wa wanachi.
"Watanzania siyo wale wa leo wala jana. Walikuwa wanakwenda kuinyima kura CCM.
"Nawaomba Watanzania wote, Uchaguzi Mkuu ujao 2020,
tukaiadabishe CCM kwa kuinyima kura kwenye sanduku la kura," Matiko
alihimiza.
Matiko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Mkoa
wa Mara, alimshauri Rais Magufuli kutolipiga 'mnada' jengo la Ikulu
lililopo Magogoni Dar es Salaam, kama ilivyowahi kukaririwa.
Badala yake ligeuzwe kuwa makumbusho ya kihistoria, litakalosaidia kuvutia watalii wengi kuzuru mjengoni pale.
"Mimi Rais sikumsikia akisema akihamia Dodoma pale atapapiga mnada. Kama ni kweli, namshauri apageuze kuwa makumbusho ya Taifa.
"Maana pale Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kakaa, Mzee
Mwinyi kakaa, Mkapa kakaa, Kikwete kakaa pale na Rais Magufuli pia kakaa
hapo," alisema.
Hata hivyo, Matiko aliyeanza kuzungumza na wanahabari saa
8:19 hadi 9:40 adhuhuri, alisema wanaamini licha ya kushinda Urais,
Chadema itaongoza pia kwa wabunge na madiwani.
"Tunakwenda kudai tume huru ya uchaguzi. Tume hii
itasababisha kura zetu za ushindi zilizopigwa zihesabiwe na kutangazwa
kama zilivyo.
"Tumejipanga," alisema Matiko huku akiwabeza wabunge,
madiwani na viongozi wengine waliohamia CCM kuwa huo ndiyo mwisho wa
siasa zao, kwani huko hawatakuwa huru kuikosoa Serikali.
No comments:
Post a Comment