HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 30, 2019

GSM WATOA GODORO KUIUA SIMBA

Na Mwandishi Wetu

KUELEKEA Mtanange wa Darby ya Kaliakoo Januari 4,2020  kati ya watani wa jadi Simba dhidi Yanga Kampuni  ya GSM Group ambao ni moja ya wadhamini wakuu wa timu ya Wananchi Yanga SC kupitia Godoro la Chapa GSM inatarajia kutoa zawadi ya godoro la nchi 5x6x8 kwa mchezaji wa Yanga atakayeibuka nyota wa mchezo baina yao na Simba.

Pambano hilo la kukata na  shoka ambalo ni la kwanza msimu huu wa Ligi Kuu Tanzania Bara, litachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao makuu ya Kampuni hiyo yaliyopo Mwenge jijini Dar es Salaam leo Desemba 30, 2019, Meneja Masoko na Mawasiliano wa GSM Group, Matina Nkurlu, amesema wameamua kutoa zawadi hiyo ili kuwapa morari wachezaji wa Yanga.

Amesema wao kama wadhamini wa Yanga ni wajibu wao kuhakikisha timu hiyo inawapa raha mashabiki wake kwa kushinda mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu na wapenzi wa soka hapa nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla. 


"Kuelekea mechi ya kukata na shoka kati ya watani wa jadi, Simba na Yanga, moja ya wadhamini wakuu wa timu ya Yanga, GSM Group kupitia godoro chapa GSM, tutatoa zawadi nono kwa mchezaji bora wa timu ya Yanga wakati wa mechi Yanga  na Simba kwa  kumzawadia godoro la nchi 5x6x8. 

 "Tunaamini zawadi hii itawaongezea wachezaji morali ya kupambana kuiwezesha Yanga kupata ushindi na hivyo kuwapa raha mashabiki wao na kuendelea kupata matokeo chanya kwa mechi zingine zijazo.

Ameongeza kuwa: "Yanga ni klabu kubwa na bora hapa nchini kama ilivyo kwa magodoro yetu Chapa GSM hivyo mashabiki wao nao wanastahili matokeo yaliyo bora uwanjani ndio maana tumeamua kutoa zawadi ili kuwapandisha mzuka wachezaji wa Yanga kuelekea mchezo huo muhimu wa Jumamosi ya Januari 4." 


Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Yanga, Fredrick Mwakalebela aliishukuru GSM Group kwa ahadi hiyo ambayo anaamini itawaongezea hamasa wachezaji wa timu yao.

No comments:

Post a Comment

Pages