Na Mauwa Mussa
Naibu Kiongozi wa Ngome ya Wanawake
wa Chama cha ACT - Wazalendo, Zahra Ali Hamadi amesema mazingira si rafiki
ya kuwashawishi wanawake wasomi kugombea nafasi za uongozi katika vyama
vya siasa.
Ameyasema hayo wakati wa mahojianao
na tasisi zisizo za kiserikali ambazo zinafanya utafiti wa kujua changamoto
zinazowakwamisha wanawake katika vyama vya siasa kugombea nafasi za uongozi
hapo ofisi ya chama cha ACT Wazalendo iliyopo Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema pamoja na kuwa serikali
imeruhusu mfumo wa vyama vingi lakini bado inawakwaza wanawake kwani
mazingira hayajawa rafiki kuwashawishi wanamke kugombea nafasi ya uongozi
kutokana Serikali iliyopo madarakani kukandamiza vyama hasa vya upinzani na
vitisho kwa viongozi wake.
Alifahamisha kuwa ili wanawake
waingie kwa wingi katika nafasi za uongozi serikali inatakiwa iweke mazingira
mazuri na hali bora ya demokrasia.
Alisema wanawake wengi hasa wasomi
wanashindwa kuingia katika harakati za siasa kutokana na kuhofia usalama wao
hasa wakati wa uchaguzi.
Pia alifahamisha kuwa kuwepo kwa
mifumo dume katika vyama vya siasa pamoja na mila na tamaduni ni miongoni
mwa changamoto zinazowanyima fursa wanawake kugombea nafasi hizo.
Hata hivyo alisema kwa mwaka 2020
wanamatarajio makubwa ya wanawake wa chama hicho kugombea nafasi za uongozi
kwani wamejipanga mapema ili kuingia katika uchaguzi.
Nae naibu katibu mkuu wa chama hicho
nd Hamad Mussa alisema ili wanawake waweze kushawishika na kuingia katika
nafasi za uongozi ni lazma serikali iweke mazingira mazuri wakati wa uchaguzi.
“Wanawake wanakabiliwa na changamoto
ya hali ya kiuchumi na kukosa utayari ambapo wengi wao hushindwa kumudu
kugombea nafasi za uongozi.”alisema Naibu Hamadi Mussa.
Hata hivyo alisema katika chama
chake ambacho kina asilimia kubwa ya viongozi wanawake akiwemo katibu mkuu wa
chama hicho ndugu Dorathon ambae ni mwanamke.
Sambamba na hilo naibu huyo alisema
chama chake kimengeza mtandao katika maeneo mbali mbali na kutoa fursa kwa
wanawake kugombea nafasi za uongozi.
Kwa upande wake muawakilishi kutoka
asasi za kiraia kutoka Zanzibar Gender Coalition Bi Asha Abdu amewataka
viongozi wa vyama vya siasa kufanya ushawishi kwa wanawake wa vyama hivyo ili
kugombea nafasi za uongozi.
Bi Asha amesema wanawake wa vyama
vya siasa wameonekana kuwa wachache katika nafasi za uongozi hasa katika vyombo
vya kutunga sheria.
Asasi zisizo za kiserikali ikiwemo
chama cha wandishi wa habari wanAwake TAMWA zinafanya utafiti katika
vyama vya siasa ili kujua changamoto zinazowakabili wanawake katika
kugombea nafasi za uongozi.
No comments:
Post a Comment