HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 05, 2019

TACCEO: Utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa ufutwe

Na Mwandishi Wetu

SIKU chache baada ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa uliosusiwa na vyama vya upinzani, Asasi za Kiraia zinazoangalia uchaguzi Tanzania, (TACCEO) kimependekeza utaratibu wa mgombea kupita bila kupingwa ufutwe.

TACCEO wamependekeza kuwa mgombea ambaye hatakuwa na mpinzani apigiwe kura ya ‘Ndiyo au Hapana’ ili kuwapa wigo mpana zaidi wananchi wa kumchagua kiongozi anayefaa.

Asasi hizo pia zimesema uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24, mwaka huu ulighubikwa na kasoro za kimfumo na kiutendaji zilizowanyima wapiga kura, wagombea na vyama vya siasa haki ya msingi ya kushiriki katika uchaguzi huo.

Akisoma tamko la TACCEO, mbele ya waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam leo, Mwenyekiti wa asasi hizo  Martina Kabisana, alisema wagombea uongozi waliondolewa katika mchakato wa uchaguzi kwa madai yasiyokubalika kidemokrasia.

Kabisana, alisema licha ya kutimiza masharti ya sheria na miongozo ikiwamo taratibu zinazotakiwa, asasi zinazounda TACCEO  na nyingine zilinyimwa vibali vya kuangalia uchaguzi huo uliofanyika Novemba 24.

Alisema Sheria ya Serikali za Mitaa sura 287, kama inavyoelekezwa na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, inaeleza kuwa asasi za kiraia zikitimiza masharti zingeruhusiwa kuangalia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 24 mwaka huu.

“Hatua hii kumeinyima haki ya kuangalia uchaguzi pamoja na kumewanyima Watanzania haki ya kujua iwapo ulifanyika kama kuaminika, huru na haki.

“baadhi ya wagombea bila kuwa na hadhi ya uongozi wa umma, walipitishwa kuongoza vitongoji, vijiji na mitaa bila kupigiwa kura; wanaongoza bila ridhaa ya wananchi, kinyume na msingi mkuu wa utawala bora wa kidemokrasia, “ alisema Martina

“Tulikuwa na mipango na maandalizi ya teknolojia, utaalam na mtaji wa kijamii kuangalia uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu kwa ufanisi nchini kote, na kisha kutoa ripoti,” alisema

Mjumbe wa TACCEO aliyeshiriki kusoma tamko hilo Buberwa Kaiza, alisema kama serikali itaendelea kuwanyima vibali vya kuangalia uchaguzi watangalia njia bora za kutekeleza wajibu wao.

Naye mmoja wa wajumbe wa TACCEO, Hebron Mwakagenda, alisema wanapendekeza serikali na vyama vya siasa vishirikiane kuhakikisha dosari zilizojitokeza hazijirudii tena kwa kuangalia mfumo wa usimamizi wa uchaguzi.

“Tunaishauri serikali kwa kushirikiana na wadau wengine, pamoja na vyama vya siasa, wakubali kuhamishia majukumu ya kuandaa na kusimamia chaguzi za serikali za mitaa kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC)” alisema

TACCEO imependekeza kuwa elimu ya uraia kwa wapiga kura, hususan katika serikali za mitaa, iwe ni suala la wakati ikiwamo vyombo vya habari, asasi za kiraia kuendelea kutoa elimu hiyo.   
 

No comments:

Post a Comment

Pages