HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 21, 2019

TANZANIA NA UGANDA ZAWEKA MKAKATI UBORESHWAJI SEKTA YA KILIMO

 Naibu Waziri wa Chakula na Kilimo, Omary Mgumba (kushoto) akisalimiana na Waziri wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda wa Uganda, Vincent Ssempijja, alipofanya ziara ya kikazi nchini humo.
 baada ya kuwasili ofisini kwa Waziri Ssempijja, jijini Kampala.


Na Mwandishi Wetu, Kampala

TANZANIA na Uganda zimekubaliana kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo, hususani zao la kahawa na korosho.

Mazao mengine yaliyowekewa mkazo ni mafuta ya mchikichi (mawese), alizeti, kilimo cha miwa na viwanda vya sukari.

Hayo yamejiri kwenye kikao cha pamoja, baina ya Naibu Waziri wa Kilimo, Omary Mgumba na Waziri wa Uganda anayeegemea Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda, Vincent Bamulangaki Ssempijja, jijini hapa.

Waziri Mgumba amesema kando ya kikao hicho kuwa, ushirikiano wa Tanzania na Uganda ni daraja la maendeleo kwa jamii.

Alikuwa kwenye ziara ya siku mbili nchini Uganda, ambapo pia alishiriki michezo ya mpira wa miguu baina ya Timu ya Wabunge wa Bunge la Tanzania na Uganda.

Alisema Septemba mwaka huu jijini Dar es Salaam, nchi hizo ziliridhia kushirikiana mbele ya Rais Dk. John Magufuli na mwenzake, Yowel Museven wa Uganda.

"Ushirikiano mwingine tuliohimiza ni kubadilishana uzoefu, ujuzi na teknolojia za kuendeleza sekta ya kiliko mazao, ufugaji na uvuvi.

"Katika  kilimo mazao, mkazo tumeweka kwenye ushrikiano wa kilimo cha korosho, kahawa, mbegu za mafuta ya michikichi," Waziri Mgumba alisema.

"Alizeti, kilimo cha miwa na uwekezaji wa viwanda vya sukari ni vipaumbele muhimu kukuza uchumi wa wananchi wetu," alisisitiza.

Katika mkutano wao huo, mawaziri hao walijadiliana kwa kina juu ya utelekezaji wa makubiliano yao.

Vilevile waliongelea kushirikiana namna ya kukabiliana changamoto za kilimo na biashara za mazao ya sekta hiyo.
"Mfumo wa masoko na sera za sekta ya kilimo, hususani kahawa hasa kutokana changamoto ya kuyumba na kushuka kwa bei ya zao hilo, katika soko la Kimataifa.

"Kuyumba kwa soko hilo inatokana na kuongezeka kwa uzalisha kwa zaidi ya asilimia 65, kwa miongo miwili iliyopita," alisema Naibu Waziri Mgumba.

Changamoto nyingine aliyoitaja ni kusokoendana na kasi, kuongezeka kwa wanywaji na watumiaji wa bidhaa za kahawa Duniani.

Kwamba, kutegemea zaidi soko la nje kwa kahawa zikiwa hazijaongezewa thamani, bado ni changamoto inayotiliwa mkazo utatuzi wake.

Waziri wa Kilimo, Mifugo, Uvuvi na Viwanda wa Uganda, Ssempijja, alisema mazungumzo yake na Waziri Mgumba yalikuwa na tija kwa maendeleo ya nchi zote.

"Tumejadiliana mikakati ya kuhamasisha unywaji wa kahawa, katika mataifa yetu, Ukanda wa Afrika Masharini na Afrika kwa ujumla.

"Tunataka Uganda na Tanzania tutengeneze soko la ndani na kikanda," alisema Waziri huyo wa Uganda.

"Hii ni kwa ajili ya kupunguza utegemezi wa soko la nje zaidi na kuinua soko kwa ujumla," alikaririwa Ssempijja.
Naibu Waziri Mgumba alikuwa Kampala kwa shughuli za kijamii, ambapo amehitimisha ziara hiyo ya siku mbili.

No comments:

Post a Comment

Pages