HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 12, 2019

TIRA: WAKULIMA JIUNGENI NA BIMA YA KILIMO

Na Betty Kangonga

WAKULIMA Nchini wametakiwa kujiunga katika vikundi ili kuhakikisha wanakata bima ya kilimo hatua itakayoweza kuwainua kiuchumi.

Akizungumza mwishoni mwa wiki, jijini Dar es Salaam kwenye mafunzo ya uelewa wa Bima kwa wanahabari, yaliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Bima (TIRA), Mshauri wa masuala ya bima, Eliya Kajiba, alisema kuwa hadi sasa ni kampuni tano tu ndizo zinazokata bima hiyo.

Kajiba alisema, bima hiyo ni mpya na bado haitambuliki kwa wakulima wengi hivyo kuna umuhimu wa kutoa elimu ili kuhakikisha sekta hiyo inajiunga na matumizi ya bima hiyo.

“Bima hii ni mpya sana kwa wakulima na hasa katika uchumi huu wa viwanda huku mahitaji yake yakiwa ni makubwa kwa sasa,” alisema.

Mshauri huyo alisema, bima hiyo inakinga upungufu wa mavuno unaosababishwa na ukame, mvua iliyozidi (mafuriko) na magonjwa ya mimea.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa Tira, Dk. Baghayo Saqware, alisema kuwa hadi sasa kati ya kampuni 29 za bima zilizopo taarifa zinaonyesha ni chini ya tano zinatoa bima hiyo.

Dk. Saqware alisema, tayari wadau muhimu wamejulishwa kuhusu mkakati huo wa kufidia hasara wanayoweza kupata wakulima.

Alisema kuwa wakulima watafidiwa kwa mfumo unaotumika duniani ambapo kuna aina mbili ambayo ni weather index  (bima ya majanga ya hali ya hewa) au (bima ya mavuno).

Mkurugenzi Mkuu huyo alisema kampuni za bima hulipa fidia pia katika majanga mengine ya kibinadamu akitolea mfano moto au uvamizi wa mifugo mashambani.

“Bila kujali sababu, bima italipa kulingana na uharibifu uliotokea, kama mkulima katumia mbegu bora, akapanda vizuri na kwa wakati na kufuata viwango vyote vinavyoshauriwa huku akiwa na matarajio ya kuvuna magunia 20 kwa mfano lakini akaambulia magunia pungufu, hapo bima itamlipa kiasi kilichopotea,” alisema. 

Hata hivyo ilielezwa kuwa kampuni za bima zinasema kuwa kikwazo cha kushindwa kutoa bima ya kilimo ni kukosekana kwa taarifa na wakulima kushindwa kujiunga kwenye vikundi ambavyo ni rahisi kuvihudumia.

No comments:

Post a Comment

Pages