MAMLAKA
ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) iko katika hatua za juu za
majadiliano na Chuo cha Ufundi Stadi wa Kilimo Henan cha nchini China
kwa lengo la kuanzisha chuo maalum cha ufundi stadi kitakachobobea
katika utoaji wa mafunzo ya ufundi stadi katika fani za Kilimo na
Mifugo.
Ujumbe
wa timu ya viongozi na wataalam 9 kutoka Chuo cha Henan, ukiongozwa na
Makamu wa Rais wa Chuo hicho, Prof. Wu Guozhao, ulikuwepo nchini kwa
siku mbili, Novemba 18 na 19 Desemba 2019 kwa ajili ya kutembelea vyuo
vya VETA na kufanya mazungumzo ya awali na Menejimenti ya VETA juu ya
mpango huo.
Timu
hiyo ilitembelea na kujionea mazingira na hali halisi ya utoaji mafunzo
katika vyuo vya VETA Kihonda Mkoa wa Morogoro kinachotoa mafunzo katika
Fani ya Ufundi wa Zana za Kilimo na Chuo cha TEHAMA cha VETA Kipawa.
Ikiwa
Morogoro, timu hiyo ilipata pia fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha
Sokoine cha Kilimo (SUA) kwa lengo la kupanua zaidi ufahamu wa mafunzo
ya kilimo yanavyotolewa nchini.
Akizungumzia
wakati wa majadiliano na ujumbe huo, Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Dk.
Pancras Bujulu alisema ana imani kubwa kuwa mpango wa ujenzi wa chuo
hicho utawavutia wengi na unagusa sekta ya kipaumbele kikubwa katika
jamii.
Alisema
asilimia kubwa ya Watanzania wanaishi kwa kutegemea kilimo na hata
wafanyakazi na wafanyabiashara wengi nchini pia wanapenda
kujishughulisha na kilimo.
“Kwa
miaka mingi watu wengi wanaulizia mafunzo ya Kilimo cha Mazao ya
Bustani, Usindikaji wa Mazao ya Chakula na hata Kilimo cha Mazao ya
Nafaka. Kwa ujumla naona kuna mahitaji mengi ya ujuzi katika eneo la
kilimo. Bila shaka mpango huu utaungwa mkono na Serikali yetu tukufu ya
awamu ya tano,” alisema Dk. Bujulu.
Alisema
VETA ina nia ya kuimarisha mafunzo katika sekta ya Kilimo na Mifugo na
miongoni mwa malengo ni kuwa na chuo mahsusi kitakachobobea na kuwa
kituo bora cha mfano katika mafunzo ya ufundi stadi kwenye sekta za
Kilimo na Mifugo.
Kwa
upande wake Makamu wa Rais wa Chuo cha Henan, Wu Guozhao amesema ni
vyema kuweka mpango maalum wa utekelezaji wa wazo hilo la kujenga chuo
kwa ushirikiano na kuhakikisha kuwa pande mbili zinauridhia kabla ya
kuanza kuutekeleza hatua kwa hatua.
“Hata
sisi tunahitaji ridhaa ya Serikali yetu. Chuo chetu kinaendeshwa kwa
fedha za serikali, tunaweza kupata msaada wa serikali kwa kiwango
fulani. VETA nanyi mnapaswa kuzungumza na serikali ili kupata ridhaa
yake na kuomba ufadhili kwa ajili ya ujenzi na uendeshaji wa chuo
hicho,” alisema Guozhao.
No comments:
Post a Comment