HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 10, 2020

Caritas watoa mikopo kwa akina mama Dar

Baadhi ya akina mama walea pekee wa kikundi cha Awape wakiwa katika picha ya pamoja Mara baada ya kupatiwa mikopo waliosimama. Waliokaa wa pili kutoka kulia ni Mkurugenzi wa Idara ya Caritas - DSM Jimbo Kuu Katoliki Christian Shembilu.



Na Asha Mwakyonde

AKINA mama walea pekee wa kikundi cha Awape wametakiwa kuzitumia fedha za mikopo walizopatiwa kwa lengo lililokusudiwa la kuanzisha biashara ndogo ndogo ili waweze kuinuka kiuchunia.

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati akikabidhi mikopo hiyo kwa akina mama hao Mkurugenzi wa Idara ya Caritas - DSM Jimbo Kuu Katoliki Christian Shembilu alisema hakuna mtu aliyefanikiwa bila kuwa na nidhamu ya fedha hivyo ni vema wakazitumia kwa lengo lililokusudiwa.

Alisema  kuna njia nyingi za kuweza kupata mikopo ikiwamo benki  lakini wao kama Caritas - Dsm wameona waanzishe mfuko ili kuwasaidia akina mama ambao wametelekezwa na wanaume huku wakiachiwa watoto wawalee peke yao.

" Hakuna mtu anayeweza kuanzisha biashara hasa kwa wakati kama huu tulionao bila kuwezeshwa na sisi Caritas -Dsm tumeona mfuko utakao wakopesha akina mama kama nyie ili muweze kuanzisha biashara na kuweza mudumu familia zenu," alisema Mkurugenzi huyo.

Aliongeza kuwa wapo tayari kuwakopesha walioenesha nia ya kuanza kufanya biashara na wale walioanza huwaongezea mtaji ili kukuza biashara zao.


Naye Mratibu Kitengo cha Jinsia na Maendeleo Caritas - Dsm  Gladys Oning'o alisema kuwa  akjna mama hao waliopatiwa mikopo ni wachache kati ya walioanza kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali wengine wamechukua kutoka Awape Saccos kwa kuwa tayari walishaanza biashara.

"Tuna Awape Saccos  na kikundi hiki cha Awape kwa ajili ya Hawa wadogo ambao wanahitaji elimu ya ujasiriamali na kuanzisha biashara," alisema Gladys.

Gladys aliongeza kuwa akina mama hao wa kikundi cha Awape  wanahitaji mafunzo,kutembelewa na kutiwa moyo ndio wanaochukua mikopo ili waendeleze biashara ndogo ndogo.

Kwa upande wake Asia Mohamedi ambaye ni mnufaika wa mikopo hiyo alisema kuwa fedha hiyo itamsaidia kukuza biashara yake ya mama lishe .

" Natoa wito kwa wanawake wenzangu ambao wanalea watoto wao bila msaada wa wanaume waliowazalisha kujakujiunga na kikundi hiki cha Awape kwani Caritas - Dsm imelenga kutusaidia na kutuinua kiuchumi,"alisema Asia.

Aidha aliushukuru uongozi wa Caritas -Dsm kwa kubuni  mikopo hii ya kuwasaidia akina mama walea pekee baada ya kutelekezwa na wanaume

No comments:

Post a Comment

Pages