Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akikagua mradi wa Nyumba 54 za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) zilizopo
wilayani Masasi mkoa wa Mtwara jana wakati wa ziara yake ya kukagua utendaji
kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kutembelea miradi ya ujenzi wa NHC katika
mikoa ya Kusini. Kulia ni Meneja Mawasiliano wa Shirika la Nyumba Muungano
Saguya. (PICHA
NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI).
Na Munir Shemweta, WANMM MASASI
Naibu Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameitaka Bodi ya Shirika la
Nyumba la Taifa (NHC) kupitia upya gharama za nyumba zake ilizojenga maeneo ya
pembezoni kwa ajili ya kuziuza.
Dkt Mabula alitoa kauli
hiyo jana wilayani Masasi mkoa wa Mtwara wakati alipotembelea mradi wa nyumba
54 zilizojengwa na Shirika la Nyumba la Taifa akiwa katika ziara yake ya
kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi katika mikoa ya Kusini pamoja na
kutembelea miradi inayofanywa na NHC katika maeneo mbalimbali nchini.
Kauli hiyo ya Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inafuatia kulalamikiwa na wabunge
wa Majimbo ya Masasi Dkt Rashid Chuachua na yule wa jimbo la Lulindi mkoani Mtwara Jerome Bwanausi kuwa pamoja na
halmashauri kuhitaji nyumba kwa ajili ya watumishi lakini gharama imekuwa kubwa
kiasi cha halmashauri na wananchi kushindwa kuzinunua.
‘’ Ni vizuri bodi ikae
iangalia namna ya kupitia upya gharama za nyumba zote zilizopo maeneo ya
pembezoni kama hizi za Masasi maana zikiachwe bila kununuliwa itakuwa ni
hasara’’ alisema Dkt Mabula.
Naibu Waziri Mabula
alisema, hata kama nyumba hizo zilizojengwa kwa ajili ya kuuza hazitanunuliwa
basi NHC iangaliae namna ya kuzipangisha na kueleza uhitaji wa nyumba katika
eneo la Masasi upo na watumisi wa serikali wanahitaji kuisha maeneo rafiki.
Hata hivyo, amezitaka
halmashauri nchini kulitumia Shirika la Nyumba la Taifa kujenga miradi ya
nyumba za watumishi kulingana na mahitaji ili kuepuka kujenga nyumba ambazo
mwisho wa siku zinaweza zisinunuliwe.
Kwa
upande wake Meneja
Mawasiliano wa Shirika la Nyumba la Taifa Muungano Saguya alisema
shirika lake
liko katika hatua za mwisho za kukamilisha mradi huo uliokuwa
umesimama kwa muda ambapo takriban milioni 600 zitatumika kuukamilisha
na kusisitiza imani yake katika kipindi cha miezi sita ujenzi
utakamilika.
Kwa mujibu wa Saguya, bei
inayolalamikiwa ya shilingi milioni 54 kwa nyumba moja inatokana na gharama
kubwa iliyotumiwa na Shirika la Nyumba la Taifa kuzijenga nyumba hizo na
kubainisha kuwa NHC iko mbioni kuzipangisha baadhi ya nyumba ambazo wananchi
wameonesha nia ya kupanga.
Katika
hatua nyingine Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo
ya Makazi Dkt Angeline Mabula alizitembea wilaya za Nanyumbu na Tunduru na
kukagua utendaji kazi katika sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya hizo.
Dkt Mabula alibaini
utunzaji mbovu wa kumbukumbu za majala ya ardhi pamoja na kiasi kidogo cha
makusanyo ya maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi ambapo aliziagiza
halmashauri za Nanyumbu na Tunduru kuongeza kasi ya makusanyo ya kodi ya pango
la ardhi sambamba na kuzingatia utunzaji majalada ya ardhi kwa kufuata taratibu
ikiwemo kuwepo mawasiliano katika majalada hayo kutoka afisa mmoja kwenda kwa
mwingine.
No comments:
Post a Comment