HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 18, 2020

DCC TABORA YAPITISHA MAPENDEKEZO YA BAJETI YA BILIONI 52 YA MWAKA UJAO

Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Komanya Kitwala (wa pili kushoto), akifungua jana kikao cha Kamati ya Ushauri ya Manispaa ya Tabora (DCC) ya kupitia na kujadili makisio ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya shilingi bilioni 52 kwa ajili ya  mwaka wa fedha ujao. (Picha na Tiganya Vincent).



Na Tiganya Vicent

WAJUMBE wa Kamati ya Ushauri ya Manispaa ya Tabora (DCC) wamepitisha makisio ya mapendekezo ya mpango na bajeti ya shilingi bilioni 52 kwa ajili ya  mwaka wa fedha ujao wa fedha.

Wajumbe hao walipitisha mapendekezo hayo jana baada ya Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora Bosco Ndunguru kuwasilisha wakati wa kikao kupitia mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2020/21.

Alisema katika mapendekezo hayo wanatarajiwa kukusanya shilingi bilioni 4.7 kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri ikiwa ni ongezeko la asilimia moja ukilinganisha na masikio ya mwaka 2019/20 ya kukusanya bilioni 4.6.

Ndunguru alisema kwa upande wa Serikali Kuu na kwa wahisani wanatarajia kupata jumla shilingi bilioni 48 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 ukilinganisha na bilioni 38.2 ya mwaka 2019/20.

Alivitaja vipaumbele vya bajeti ijayo kuwa ni uendelezaji wa jengo la utawala ambalo limetengewa milioni 200, kutenga fedha milioni 70 kwa ajili ya ununuzi wa ardhi ekari 140  za uwekezaji.

Nduguru aliongeza kuwa vipaumbele vingine ni kutenga milioni 50 kwa ajili ya fidia kwa wananchi ili kutatua migogoro, milioni 84 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya Shule za Msingi na Sekondari na ununuzi wa taulo kwa ajili ya wanafunzi wa kike na milioni 200 kwa ajili ya ujenzi wa Shule mbili za Kidato cha Tano na Sita.

Aliongeza kuwa kiasi cha milioni 445 kinatarajiwa kutolewa kama mikopo ya vikundi vya vijana , wanawake na walemavu na milioni 117 zimetengwa kwa ajili ya shughuli za lishe.

Ndunguru alisema kwa upande wa miradi wamependekeza shilingi milioni 580 zitumike katika miradi ya maendeleo kwenye Kata 29 za Manispaa ya Tabora  na bilioni 1 zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya Halmashauri hiyo

No comments:

Post a Comment

Pages