Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile (kushoto) akisikiliza taarifa ya mkoa
kutoka kwa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga wakati wa
ziara yake ya siku mbili mkoani Iringa kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo
ya Jamii mkoani humo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile akisalimiana na kuzungumza na mzee
aliyekutana naye akipatiwa huduma katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa wakati
wa ziara yake ya siku mbili mkoani humo kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo
ya Jamii.
Na Mwandishi Wetu, Iringa
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile amemuagiza Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga kuhakikisha anapata taarifa
ya utoaji wa dawa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa.
Agizo hilo limekuja mara baada ya
ziara ya yake mkoani humo alipotembelea hospitali hiyo kujionea utoaji wa
huduma za afya kwa wananchi na kushuhudia mmoja wa mama aliyejifungua
Hospitalini hapo kupewa dawa mara moja badala ya mara tatu kama iilivyoandikwa
na Daktari.
Dkt. Ndugulile amesema kuwa amekasirishwa
na utendaji kazi wa manesi katika wodi ya Mama na Mtoto kwa kutozingatia utoaji
huduma hasa kuhakikisha wazazi na watoto wanapewa dawa kwa wakati zinazotakiwa
na kwa idadi sahihi.
Ameongeza kuwa lengo la mgonjwa
kupewa huduma ni kuhakikisha anapona na sio kufanya aendelee kupata tabu na
shida hivyo Serikali ya Awamu ya Tano imewekeza fedha nyingi katika kuhakikisha
Sekta ya Afya inaboreshwa nchini.
"Haiwezekani mgonjwa kanunua
dawa zake kwa fedha zake lakini bado hata hamzingatii kumpatia dawa mnategemea
ataponaje” alisema Dkt. Ndugulile.
Aidha Dkt. Ndugulile ameutaka
uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kuhakikisha wanaratibu utoaji
wa huduma hospitalini hapo ili kuepukana na malalamiko ya wagonjwa na kupoteza
imani ya wananchi kwa Hospitali hiyo.
"Tukiendelea hivi tutaondoa
imani kwa wananchi wetu katika utoaji wa huduma za afya sisi tunatakiwa kutoa
huduma kwa wananchi na sio kuwapa kero wananchi" alisema Dkt. Ndugulile.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Iringa Dkt. Atupele Mwandiga amemuahikikishia Naibu Waziri Dkt.
Ndugulile kusimamia utoaji huduma katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa
na kusimamia vilivyo ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma inayostahili.
Ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya
tano imetoa kiasi cha Billioni 7 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya na
maboresho katika Zahanati na vituo vya Afya mkoani humo katika kuhakikisha inaboresha
Sekta ya Afya hivyo watasimamia Sekta hiyo kikamilifu.
"Mhe. Naibu Waziri
tutahakikisha hatutopoteza imani ya wananchi katika utoaji huduma za afya na tutatendea
haki rasimali fedha tulizopewa na Serikali katika kuboresha Sekta ya Afya
Mkoani kwetu" alisema Dkt. Atupele
Wakati huo huo Dkt. Ndugulile
ametembelea na kujionea utendaji kazi utoaji wa huduma kwa wananchi katika
Ofisi ya Bima ya Afya (NHIF), Kampeni ya masuala ya Lishe, Kiwanda cha Ruaha
Milling na ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Kilolo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Faustine Ndugulile yuko katika ziara
ya siku mbili mkoani Iringa kukuagua shughuli za Afya na Maendeleo ya Jamii
mkoani humo.
No comments:
Post a Comment