HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 13, 2020

Kitabu cha Wakati Taabu itakapokoma chazinduliwa

Mchungaji wa Kanisa la Waadventista Wasabato , Mashariki ya Kati Tanzania, Amos Lutebekela, akionesha kitabu cha Wakati Taabu itakapokoma alichokizindua mwishoni mwa wiki.
Muamini Piliphina Werema.
 
 
Na Nwandishi Wetu, Bagamoyo
 
 
WATANZANIA wametakiwa kuondokana na hofu katika maisha yao kwa kusoma kitabu cha Wakati Taabu itakapokoma kilichozinduliwa hivi karibuni Wilayani Bagamoyo.
 
Wito huo umetolewa hivi karibuni na viongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato katika katika uzinduzi wa kitabu hicho uliofanyika katika kanisa hilo lililoko Bagamoyo mkoani Pwani.
 
Mchungaji wa Kanisa hilo, Mashariki ya Kati Tanzania, Joseph Chengula alisema ujumbe wa kitabu hicho ni wa ulimwengu mzima hivyo kila mmoja anatakiwa akipate kwa ajili ya kupata ujumbe wa neno la Mungu hasa kwa waliogubikwa na matatizo mbalimbali yaliyoko katika jamii.
Chengula alisema jamii inatakiwa kujiandaa na kumpokea Yesu kwa mara nyingine baada ya mapito ya aina yake ambayo yamewavunja moyo na kuwakatisha tamaa katika maisha yao.
 
“Jamii zote duniani zimevunjika moyo, vifo, njaa, matatizo ya kijinsia hivyo kwa matatizo kama haya, jamii inatakiwa ipate uponyaji kutoka katika kitabu tulichokizundua jana,” alisema Mchungaji Chengula.
 
Chengula alisema gharama ya kitabu hicho ni shilingi 2,500 kiasi ambacho kinaweza kufanikishwa na kila mtanzania mwenye kihitaji kupata ujumbe wa neon la Mungu.
 
Naye Katibu Mkuu wa Jimbo la Mashariki Kati, Mchungaji Amos Lutebekela alisema kitabu cha utume kama hicho hutokea kila mwaka hivyo mwaka huu kitabu hicho kimekuja kwa ajili ya uponyaji wa jamii kuhusu matatizo mbalimbali yanayowakabili.
 
“Kitabu kimekusudia kuonesha jinsi dunia ilivyojaa taabu ambayo itaondoshwa kwa Yesu Kristo ambaye alikufa na kufufuka kisha kupazwa mbinguni,” alisema Mchungaji Lutebekela.
 
Muinjilisti Virginia Said alimshukuru Mungu kwa matukio mawili yaliyofanyika jana kanisani kwao Bagamoyo, mojawapo ni uzinduzi wa kitabu na uzinduzi wa Kanda mpya ya Bagamoyo.
 
Alisema kitabu kinatoa wito kwa jamii kufuata nyayo za Yesu Kristo katika taabu wanazopitia ambazo zitakoma ikiwa tutafuata maagizo yake na baadaye tutasogezwa karibu na Mungu.
 
Mkurugenzi wa Huduma za Uchapaji Union ya Kusini mwa Tanzania, Mchungaji John Nyaibago alisema kitabu hicho kinaponya matatizo mbalimbali katika jamii yakiwemo ya unyumba, malezi ya watoto na mengineyo mengi, hivyo ni kazi ya jamii kukinunua kitabu ili kuondokana na madhila waliyonayo.
 
Mchungaji Nyaibago alisema Mungu atayaondoa matatizo waliyonayo binaadam lakini sasa wamejiandaaje kupokea uponyaji huo ambao utakuwa msaada kwao.
 
Muumini wa Kanisa hilo wilayani Bagamoyo, Piliphina Werema, alionesha furaha ya ujio wa kitabu hicho kwani jamii imegibikwa na matatizo mengi ambayo yanakatisha tamaa katika maisha yao, hivyo wakinunue kitabu hicho ili warudishe faraja yao iliyopotea.
 
Uzinduzi wa kitabu hicho ulikwenda sambamba na uzinduzi wa jimbo la Bagamoyo ambalo ni la 10 kati ya Kanda ya Mashariki na Kati (ECT) ambayo ni Morogoro, Gairo, Ifakara, Mwenge, Magomeni, Manzese, Kinondoni, Kibaha na Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Pages