HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 16, 2020

Makocha na Wachezaji Wazawa Wasidharauliwe!

Mkwasa
Na Bryceson Mathias, Turiani
 
KAMA Viongozi wa Michezo hasa wa Klabu Kubwa za Mpira wa Miguu nchini, zikiwemo Simba, Yanga na Azamu, hawataamka usingizini wakaondokana na Kasumba ya kuwadharau makocha na wachezaji wazawa, wataendelea kuwa kichwa cha Mwenda wazimu michezoni.
Ushauri huo umetolewa na baadhi ya wadau wa michezo Turiani Mvomero ikiwa ni siku chache baada ya vilabu vikubwa vinavyofundishwa soka na wageni ambapo bila aibu vilijikuta vikibugizwa mabao mfululizo na timu zinazofundishwa na Wazawa.
Atoa mifano ya hivi karibuni mbali ya iliyopita, Abubakar Sadan, alidai, “Ubora wa Majengo si Kigezo cha Ufaulu wa wanafunzi! Majuzi kwa macho na masikio yetu, tuliona Nyama ya ‘’Simba inayofundishwa na Mzungu iliungwa Sukari badala ya Chumvi na Mtibwa inayofundishwa na Mzawa, Shabani Katwila.
“Timu ya Wananchi Yanga inayofundishwa na Mgeni, ambayo siku kadhaa ilikuwa katika hali mbaya na kuokolewa na Mzawa, Charles Bonfarce Mkwasa, iilicharazwa bakora za Miwa na  Kagera Sugar, inayofundishwa na Mzawa, Meck Mexime”. Alisema mdau huyo.
Aliongeza katika Ndinga la Watani wa Jadi Yanga na Simba hivi karibuni, Mkwasa (Mzawa) alifanikiwa kurejesha Heshima ya Yanga iliyokuwa inadorora na kuidhibiti Simba inayofundishwa na Mgeni.
Alisema, Timu ya Costal Union ya Tanga inayofundishwa na Mzawa, Juma Mgunda, na hivi karibuni ilivuruga viburusho vya Azam visitengenezwe inayofundishwa na Mgeni, jambo linaloonesha makocha wazawawako vizuri, ila wanadharauliwa.
Pamoja na kwamba viongozi wetu kila siku wanashauri na kutusisitiza ‘tupende bidhaa zetu na kwamba ‘turudi nyumbani kumenoga! Kauli hiyo kwa viongozi wetu wa michezo nchini imekuwa ni kama kumpigia mbuzi gitaa maana hawezi kucheza bali atapanda kwenye miti hata yenye miiba!
Aidha, Amina Juma, alidai tatizo hilo ndilo lililoko hata kwa wachezaji ambapo wachezaji wazawa wanadharauliwa lakini mara kadhaa ndio wanaoziokoa timu zao kwenye michezo migumu na wachezaji wenye kipaumbele wakiwa hawakufanya chochote!
Akihitimisha mwanadada wa Morogoro mjini na mepenzi wa soka alisema, kitu kingine kinachozitesa timu hizi ni kuchukuliana wachezaji, leo huyu katoka Yanga amekwenda Simba, Kesho anatoka Simba anarudi Yanga, Kesho kutwa Azam tabia hiyo ni hatari ndani mwake hakuna Uzalendo.

No comments:

Post a Comment

Pages