Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akionyeshwa mchoro wa nyumba na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NMB, Ruth Zaipuna, wakati wa hafla ya uzinduzi wa mikopo ya ujenzi wa nyumba uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Mkuu wa Wateja Wadogo, Wafanyabiashara Wadogo na wa Kati, Filbert Mponzi. (Na Mpiga Picha Wetu).
NA SALUM MKANDEMBA
WAZIRI
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, amezindua huduma mpya
ya mikopo ya fedha za ujenzi ijulikanayo kama ‘NMB Nyanyua Mjengo’, inayotolewa
na Benki ya NMB, huku akilitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kushirikiana
na benki hiyo.
Uzinduzi
wa NMB Nyanyua Mjengo, huduma inayokwenda kuwa jawabu la changamoto za ujenzi
wa ‘kuungaunga,’ ulifanyika Makao Makuu ya NMB, ambako Waziri Lukuvi
aliitaja kama chachu katika upatikanaji wa makazi mapya 200,000 kwa kila mwaka,
kulingana na mahitaji ya kitakwimu.
Akizungumza
katika uzinduzi huo, Waziri Lukuvi alibainisha kuwa, aina hiyo ya mikopo ni
mwarobaini wa changamoto zote za upatikanaji wa nyumba bora na za kisasa
miongoni mwa wananchi, na kwamba NHC inapaswa kuhamasisha wateja wao kuchangamkia
fursa zinazokuja na NMB Nyanyua Mjengo.
“NHC
inapaswa kushirikiana na NMB, kipato cha wananchi kwa sasa kiko chini,
kuwakopesha nyumba zilizojengwa mahali pamoja ni kuwatisha mzigo, kwa hiyo
wanapaswa wachukue wananchi wanaowasubirisha ujenzi kwa muda mrefu na
kuwapeleka NMB, wapate mikopo na kujenga wenyewe,” alisema.
Waziri
Lukuvi alisema takribani Hati za Viwanja milioni 1 zimetolewa na Wizara yake,
lakini wamiliki wake wengi hawana uwezo wa ujenzi wa makazi katika viwanja
hivyo na NMB inapaswa kuwafikia ili kuwafungulia fursa za mikopo yenye riba
nafuu na ya muda mrefu.
Akizungumza
kwa niaba ya NMB, Filbert Mponzi ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Wateja Wakubwa
na wa Kati wa benki hiyo, alisema wamejipanga kukidhi mahitaji ya mikopo ya
fedha kwa wamiliki wa hati za viwanja kote nchini, lengo likiwa ni kufanikisha
utimilifu wa ndoto za kumiliki makazi bora.
Mponzi
alifafanua kuwa, mmiliki wa kiwanja anaweza kupata mkopo wa NMB Nyanyua Mjengo
kuanzia Sh. Mil. 10 hadi 200, ambako mkopaji atarejesha katika kipindi cha hadi
miaka 15 kwa riba nafuu, vigezo vya upataji mkopo vikiwa ni hati halisi na
uwezo wa kifedha kufanya marejesho.
Naye
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa NMB, Ruth Zaipuna, alimpongeza Waziri Lukuvi na
Serikali ya Awamu ya tano kwa ujumla kwa jitihada za kurasmisha makazi, kupima
viwanja na kutoa Hati kwa wakati, yote yakilenga kuwawezesha wananchi kupata
umiliki na makazi bora na ya kisasa.
Zaipuna
aliwataka wananchi kuchangamkia huduma yao hiyo, kwani NMB wamejipanga na wana
fungu la kutosha linalofikia kiasi cha Sh. Bil. 23 zilizotengwa kufanikisha
mikopo ya NMB Nyanyua Mjengo na kwamba kiasi hicho kinaweza kuongezeka
kulingana na mahitaji ya wateja.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mikopo ya Nyumba ya Tanzania
Mortgage Refinance (TMRC), Oscar Mgaya, aliipongeza NMB kwa ubunifu uliozaa
huduma hiyo ya mikopo, aliyoiita suluhu ya changamoto za ujenzi na nguvu ya
ziada kwa wakopaji.
Mgaya
aliongeza kuwa, wao kwa upande wao kama wawezeshaji, wamevutiwa na kuweka
utayari wa kufanikisha hilo kwa kuiongezea nguvu NMB katika kupata fungu la
kutosha kutoa mikopo ya muda mrefu, ili kurahisisha mpango wa ukopeshaji kwa
wananchi wa kada zote.
No comments:
Post a Comment