Na Mwandishi Wetu
Uongozi wa Shule ya Mbezi Beach Secondary, Dar es Salaam, umesema hatua ya shule hiyo kupata alama mbili tu za daraja ziro (0), wakati zikiwa zipo shule nyingine ambazo zimepata hadi ziro 75, katika matokeo ya Mitihani ya Kidato cha nne ya mwaka huu, ni ishara kwamba shule hiyo bado ipo kwenye kiwango bora cha ufundishaji.
Akizungumza na baadhi ya wazazi wa wanafunzi, Meneja wa shule hiyo Dk. Prosper Kiramuu Mbowe, amesema, licha ya kuwa katika matokeo hayo shule imepata wanafunzi wawili wa daraja 0 lakini inajivuna kwamba imeweza kupata ufaulu wa wanafunzi kumi katika daraja la kwanza na kupata 49 daraja la pili, 68 daraja la tatu na 81 wa daraja la nne.
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani Tanzania, miongoni mwa shule zilizopata daraja ziro nyingi ni pamoja na Jitegemee iliyopata ziro 75, Azania ambayo imepata ziro 26, Green Acres ziro 18, Africana ziro nane, Makongo ziro saba, Jordan ziro 9 na Kawe Ukwamani ziro 39.
Akitangaza matokeo ya upimaji kitaifa darasa la nne, kidato cha pili na cha nne ya mitihani iliyofanyika Novemba 2019. Katibu Mkuu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania, Dk. Charles Msonde, alisema kwa upande wa matokeo ya kidato cha nne ufaulu umeongezeka kwa asilimia 1.4 kutoka ule wa mwaka 2018, lakini karibu nusu au asilimia 48.6 ya watahiniwa wote wa mwaka 2019 wamepata daraja la nne.
"Ni kweli mitihani ya mwaka 2019 ilikuwa na ushindani mkubwa, lakini kutokana na shule yetu kuwa na walimu hodari tumeweza kupata ufaulu wa kuridhisha, tukijilinganisha na shule kadhaa ambazo wakati sisi tuna divisheni ziro mbili wenzetu wamefika hadi ziro 75",
Sisi lengo letu ni kuhakikisha shule yetu inatoa kiwango bora cha elimu kwa watoto na uwezo wa kufanya hivyo tunao, jambo la msingi ni kwa ninyi wazazi na wananchi wengine kwa jumla kuendelea kutuamini na kutuunga mkono ili tuweze kutumiza azma hii ambayo pia ni muhimu kwa Taifa la Tanzania", alisema Dk. Prosper.
"Kama mnavyojua pamoja na kwamba lengo letu ni kutoa mchango wetu kwa taifa katika sekta ya elimu, lakini wapo watu ambao kwa kuhofu ushindani wakati mwingine hujaribu kutumia mbinu ovu hata kueneza uongo katika jamii kwa lengo la kuchafua na kushusha hadhi ya shule yetu, maana mkumbuke hizi shule zetu binafsi licha ya kwamba lengo kuu ni kutoa huduma lakini pia ni biashara", alisema Dk. Prosper.
Aliwaomba wazazi kuepuka kusikiliza maneno yanayoweza kutolewa na watu wasioitakia mema shule hiyo badala yake, wawe wanajipa muda wa kufuatilia kwa karibu kila jambo linalohusiana na shule hiyo kwa kuwa uongozi wa shule upo tayari wakati wote kutoa taarifa sahihi hasa kwa watu sahihi.
No comments:
Post a Comment