TAMASHA la Mbio za Kuadhimisha Siku ya Mapinduzi ‘Mapinduzi
Day Track Meet’ linatarajiwa kufanyika Januari 12 Uwanja wa Sheikh Amri Abeid
jijini Arusha likishirikisha mikoa mbalimbali.
Tamasha hilo limeandaliwa na Taasisi ya Gidabuday Sports
Tourism Foundation (GSTF), kwa kushirikiana na Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha
(ARAA), na kuwezeshwa na kampuni ya Infinix.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu (CEO), wa GSTF, Eva Baltazar Gidabuday,
tamasha hilo litakuwa na mbio za uwanjani ‘Track and Field’ sambamba na zile za
kujifurahisha za Kilomita 10 ‘Fun Run’.
“Maandalizi yanakwenda vema na usajili wa washiriki
unaendelea kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kwa Sh. 5,000. Tayari baadhi ya
wakimbiaji wakubwa wamesema watajitokeza kupima mida yao kama vile Alphonce
Simbu, Gabriel Geay, Failuna Matanga na pia wanariadha kutoka mikoa ya jirani
kama Kilimanjaro, Manyara, Tanga pia Zanzibar wametupigia kuelezea nia yao ya
kutaka kushiriki na tunawakaribisha sana,” alisema Eva.
Eva, alizitaja mbio za uwanjani zitakazoshindaniwa siku hiyo
ni mita 5,000, 800, 200, 400x4 Kupokezana Vijiti na Kuruka Chini kwa Wanaume na
Wanawake.
Mtendaji huyo, alibainisha kuwa hakutakuwa na zawadi katika
mbio hizo, lakini kwa upande wa uwanjani kuna hamasa imetolewa na Rais wa
Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Anthony Mtaka kwa washindi watatu wa kila
tukio.
Alisema katika kuhamasisha zaidi mbio za uwanjani, Rais wa RT
atatoa Sh. Kwa mshindi wa kwanza, Sh. 60,000 mshindi wa pili na Sh. 40,000 na mshindi
wa tatu 20,000.
Aidha, Mtendaji huyo wa GSTF, alisema wako kwenye hatua nzuri
klabu moja kutoka Colorado Marekani, kuwapa nafasi baadhi ya wanariadha
watakaofanya vizuri kwenda kushiriki mbio mbalimbali za uwanjani zenye fursa ya
kufuzu kwa Olimpiki Tokyo 2020.
Ikumbukwe, hivi karibuni Mtaka aliitaka mikoa mbalimbali
kuandaa mbio za kupokezana ‘relays’ ili kupata wachezaji watakaunda timu ya
Taifa kwa ajili ya kusaka viwango vya kushiriki Olimpiki Tokyo.
No comments:
Post a Comment