HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 14, 2020

TAKUKURU PWANI YATEKELEZA AGIZO LA RAIS KWA KUFUATILIA NA KUREJESHA FEDHA ZA KOROSHO ZILIZOIBWA NA VIONGOZI WA AMCOS


Ndugu waandishi wa habari,
Mtakumbuka kuwa msimu wa korosho uliopita wa 2018/2019 kulikuwa na ubadhirifu mkubwa wa pesa za wakulima ambapo Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mwezi Oktoba 15, 2019 wakati wa Mkutano wa hadhara na wananchi wa wilaya ya Ruangwa Mjini, mkoani Lindi aliagiza TAKUKURU na vyombo vingine vya dola kufuatilia malipo ya wakulima wa korosho wanaodai vyama vya msingi. 

Katika ufuatiliaji huu,TAKUKURU mkoa wa Pwani ilibaini kuwa baadhi ya viongozi wa vyama vya msingi na bodi ya mazao mchanganyiko walifanya ubadhirifu kwa namna mbalimbali na kupelekea wakulima wengi kukosa malipo yao na wengine kulipwa zaidi ya walivyostaili. 

Kupitia agizo hilo, Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa mkoa wa Pwani inapenda kuujulisha umma wa watanzania kuwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi Oktoba mpaka Desemba, 2019 pamoja na kufanya kazi nyingine kadiri ya majukumu yake kisheria imeweza kuokoa na kurejesha jumla ya kiasi cha fedha shilingi Milioni Mia mbili kumi na saba, laki nne themanini na moja elfu mia nne tisini na nane ( Sh. 217,481,498.00) ambazo zililipwa kwa makosa na baadhi ya viongozi wa bodi za vyama vya ushirika (AMCOS) mkoa wa Pwani na Bodi ya mazao mchanganyiko. Fedha hizi zimerejeshwa katika wilaya za Mkuranga, Kibiti, Rufiji na Kisarawe.
1
Aidha kati ya shilingi 217,481,498.00 zilizookolewa kiasi cha shilingi Milioni sitini na saba laki tisa na elfu nane mia tisa hamsini na nane (Shs. 67,908,958.00) kimelipwa kwa wakulima waliostahili kwa wilaya ya Kibiti na Shilingi 16,275,000/= kwa wilaya ya Rufiji. Kwahiyo jumla ya shilingi 84,183,958/= zimerejeshwa kwa wakulima. Hata hivyo uhakiki bado unaendelea ili wakulima wote walioonewa waweze kulipwa stahili zao kwa wilaya zote. 

Mbinu zilizotumika katika kuiba au kufanya ubadhirifu wa fedha hizo ni pamoja na kuwalipa baadhi ya wakulima malipo mara mbili kwa mzigo mmoja wa korosho yaani kufanya “Double Payments”, lakini pia kuna baadhi ya wakulima waliopeleka mazao yao kwenye vyama vya msingi na hawakulipwa fedha zao kwa kutoonekana kwa nyaraka za mapokeo ya mazao yao katika ofisi za vyama vya msingi. 

Ndugu waandishi wa habari, 
 Pamoja na kujeresha fedha hizo za wakulima wa korosho, TAKUKURU mkoa wa Pwani kwa kipindi cha Septemba – Desemba, 2019 ilitekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria kama ifuatavyo; 

UCHUNGUZI NA MASHITAKA 

Katika kipindi hiki kupitia kazi za uchunguzi, Ofisi ilipokea malalamiko 178 kati ya hayo malalamiko 120 uchunguzi wake unaendelea katika hatua mbalimbali na malalamiko 58 yalionekana kuangukia katika sheria nyinginezo hivyo walalamikaji walishauriwa na kuelekezwa sehemu husika kwa lengo la kutatua kero zao. 

Pia, katika kipindi hicho ofisi ilifungua kesi mpya Tisa (9) katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Pwani na kufanya jumla ya kesi zilizoendeshwa katika mkoa huu kwa kipindi hicho kuwa kesi 33 katika mahakama mbalimbali za mkoa wa Pwani. Aidha kesi zilizotolewa hukumu na kushinda ni kesi Tano (5) kwa washitakiwa kuamuliwa kufungwa jela au kulipa faini. Washitakiwa katika kesi nne waliamua kulipa faini na hatimaye washitakiwa kuachiwa. Mshitakiwa katika kesi ya tano alifungwa jela miaka mitatu kwa kushindwa kulipa faini ya shilingi Milioni moja na laki tano (1,500,000/=). Kesi nyingine bado zipo katika hatua mbalimbali mahakamani na zinaendelea kusikilizwa. 

ELIMU KWA UMMA. 

Ndugu waandishi wa habari,
Katika kuelimisha umma, TAKUKURU mkoa wa Pwani ilijikita kuelimisha umma juu ya madhara ya Rushwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Novemba, 2019 na pia tulijikita kuelimisha umma juu ya kampeni kubwa mbili zenye lengo la kuondoa Rushwa nchini. 

2
Kampeni hizo ni “KAMPENI YA UTATU” ambayo ni ushirikiano wa makundi matatu muhimu katika mapambano dhidi ya Rushwa za barabarani na kupunguza ajali nchini, makundi hayo ni TAKUKURU wenye dhamana ya mapambano dhidi ya Rushwa, JESHI LA POLISI wenye dhamana ya kusimamia sheria za Usalama barabarani na WADAU ambao ni watumiaji wa vyombo vya usafiri barabarani, waandishi wa habari, madereva wa magari yote wakiwemo daladala na bodaboda na madereva wa mabasi ya mikoani. 

Kampeni ya pili ni kampeni ya “VUNJA UKIMYA, KATAA RUSHWA YA NGONO” ambayo ni kampeni yenye lengo la kuamsha umma juu ya kupambana na Rushwa ya aina hii kwani watu wengi wanaombwa Rushwa ya aina hii lakini wamekuwa wazito kutoa taarifa kwa kuogopa aibu kwa jamii. Rushwa hii ina madhara makubwa sana kwa jamii na inadhalilisha na kuondoa utu wa mtu, inasababisha kifo kutokana na magonjwa na msongo wa mawazo, inatweza heshima ya mtu mbele ya jamii, inasababisha kupatikana wataalam wasiofaa, inaharibu uchumi wa nchi kwa kuwa inaathiri rasilimali muhimu kwa ajili ya maendeleo ya nchi. 

Watu wengi hasa wanafunzi vyuoni ni wahanga wa Rushwa hii. Hivyo Taasisi imedhamiria kumaliza kabisa tatizo la Rushwa ya Ngono nchini kwa kushirikisha wadau wote kwani Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na. 11/2007 Kif. Cha 25 kinakataza mtu yeyote mwenye mamlaka au madaraka kutumia mamlaka au madaraka yake kulazimisha au kuweka sharti la kupata ngono kutoka kwa mtu anayemhudumia ili aweze kutekeleza wajibu wake katika kutoa ajira, kupandisha cheo, kutoa haki yoyote au huduma yoyote ambayo iko katika mamlaka yake. 

Katika kufikisha ujumbe wa kampeni hizo mbili na kupeleka ujumbe katika uchaguzi wa serikali za mitaa ofisi iliweza kutoa elimu ya Rushwa kwa njia mbalimbali za uelimishaji ambapo semina 179 zilitolewa, mikutano 126 imefanyika, klabu za wapinga rushwa 35 zilifunguliwa na klabu 137 ziliimarishwa. Pia makala 18 zenye kueleza maudhui ya Rushwa kwa jamii ziliandaliwa na taarifa 7 zimetolewa kwa vyombo vya habari. Aidha uelimishaji huo umeweza kuwafikia jumla ya wananchi 12,320. 

3
UZUIAJI RUSHWA 

Ndugu Waandishi wa Habari,
Katika eneo la Uzuiaji Rushwa tulifanya warsha 14 katika eneo la manunuzi ya umma baada ya kubaini mapungufu kadhaa katika taratibu za manunuzi ya umma kulikokuwa kunafanywa na maafisa wa Halmashauri zetu na kusababisha serikali kupoteza fedha. Hii ilitokana na uchambuzi wa mfumo katika eneo hili uliofanyika robo ya mwaka uliopita yaani Julai-Septemba, 2019.
Katika warsha hizi zilizofanyika tumekubaliana na kuweka mikakati ya kuhakikisha kuwa taratibu za manunuzi ya umma zinazingatiwa hususani wakati ambapo miradi mingi ya serikali inatumia FORCE ACCOUNT katika utekelezaji wa miradi, hivyo ni matarajio ya Taasisi kuwa mapungufu yaliyoainishwa hayatajitokeza tena. 

Aidha tulifanya warsha na wadau wa ukusanyaji wa mapato ya serikali, kwani robo ya mwaka uliopita tulibaini kwamba kuna mianya mingi ya upotevu wa mapato katika huduma za ukusanyaji wa mapato ya serikali kupitia halmashauri zetu. Hivyo tulipofanya warsha hii tuna imani kuwa wadau watazingatia tuliyokubaliana ili kuondoa mianya ya uvujaji wa mapato hayo. Moja ya makubaliano ni pamoja na mawakala kutokukaa na fedha walizokusanya kwa muda mrefu, kuwe na taratibu za kuweka benki fedha hizo pindi zinapokusanywa, lakini pia tulikubaliana kuwe na ufuatiliaji wa karibu zaidi wa matumizi ya “POS Mashine” ili kupunguza udanganyifu. 

UFUATILIAJI WA MIRADI 

Ndugu waandishi wa habari,
Mtakumbuka kuwa ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha kuwa miradi ya maendeleo katika nchi yetu inakuwa na tija na kuleta matunda yaliyokusudiwa. Katika robo hii ya mwaka tumekagua jumla ya miradi ya maendeleo 13 katika sekta za ujenzi, barabara na Afya. Miradi hiyo ina thamani ya shilingi Bilioni mbili milioni mia tano therathini na saba laki tisa na elfu kumi na mbili miambili na hamsini na mbili na senti therathini (Sh. 2,537,912,252.30).
Aidha katika ufuatiliaji wa miradi hiyo baadhi ya miradi ilibainika kuwa na mapungufu kama vile miradi kutokamilika kwa sababu mbalimbali ikiwemo fedha kuhamishwa kupelekwa kwenye miradi mingine kinyume na taratibu, pia miradi kuwa na gharama kubwa za utekelezaji wake ukilinganisha na uhalisia wa kazi walizofanya. 

4
Kwa mfano katika wilaya ya Mafia kuna choo cha nje kimejengwa katika jengo la Ikulu ndogo ya wilaya ya Mafia kwa Shs. 32,000,000/= lakini ukiangalia “value for money” haipo. Kutokana na mapungufu kama hayo, miradi mitatu uchunguzi wake umeanzishwa, na miradi iliyobaki tumefanya vikao na wadau kwa lengo la kuweka mikakati ya kurekebisha kasoro zilizobainika, 

MIKAKATI YETU KWA KIPINDI CHA JANUARI MPAKA MACHI 2020

Ndugu Waandishi wa Habari,
Kama ilivyo Dira ya Taifa kuelekea uchumi wa viwanda na kama mnavyofahamu Rushwa ni kikwazo kwa nchi kufikia uchumi wa viwanda, TAKUKURU mkoa wa Pwani imedhamiria kufuatilia na kuchunguza vitendo vyote vya Rushwa vinavyokinzana na dira ya taifa kuelekea uchumi wa viwanda kwani mnafahamu mkoa wetu ni moja ya mikoa iliyoitikia kwa kiwango kikubwa juu ya ukuzaji wa uchumi wa viwanda nchini. Kwa msingi huo ni lazima kuhakikisha viwanda hivi vinalindwa ili kuleta matunda kwa mtanzania. 

Aidha kama mnavyofahamu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani. Kwa kutambua hilo TAKUKURU mkoa wa Pwani imejipanga kufuatilia hatua zote za mchakato wa uchaguzi huu ili kubaini vitendo vya Rushwa na kuchukua hatua zinazostahili kwa wote watakaobainika kujihusisha na Rushwa katika uchaguzi huu. Rushwa ni kikwazo kwa Tanzania kupata viongozi waadilifu hivyo ni jukumu la TAKUKURU kuhakikisha kuwa viongozi wanaochaguliwa wanachaguliwa bila kuhusisha vitendo vya Rushwa ili kupata viongozi wenye nia ya dhati ya kumkomboa mtanzania. Pamoja na mambo mengine TAKUKURU itafanya yafuatayo katika kipindi cha Januari hadi Machi, 2020:
  •   Kufikisha elimu ya madhara ya Rushwa kwa wananchi wote mpaka ngazi ya kijiji ili waone umuhimu wa kuchagua viongozi waadilifu watakaokuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.
  •   Kufuatilia michakato yote inayoendelea kuelekea uchaguzi mkuu, ikiwa ni pamoja na kubaini wale wote wanaoanza kampeni kinyume na taratibu.
  •   Kuendeleza kampeni ya UTATU kwa kushirikisha wadau wote muhimu katika mapambano dhidi ya Rushwa za barabarani ili kuondoa rushwa barabarani na kupunguza ajali nchini.
  •   Kufanya ufuatiliaji wa mikakati na malengo yaliyowekwa katika warsha zilizofanywa katika robo hii ya mwaka ili kutathmini utekelezaji wake, hii itasaidia kuziba mianya ya Rushwa iliyobainishwa wakati wa chambuzi za mfumo zilizofanywa na hivyo kuleta tija.
  •   Kuendelea kupokea malalamiko ya vitendo vya Rushwa na kufanyia kazi na kupitia uchunguzi kuwafikisha mahakamani wale wote watakaothibitika kutenda makosa ya Rushwa kinyume na Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na: 11/2007.
    5
 Kuhakikisha fedha zilizofanyiwa ubadhirifu kwenye zao la korosho kwa msimu wa 2018/2019 zinaokolewa zote na kurejeshwa kwa wakulima waliostahili. Hii ni kuendeleza utekelezaji wa maagizo ya viongozi wetu wa kitaifa. 

WITO WA TAKUKURU KWA WANANCHI 

Ndugu waandishi na wananchi,
Naomba kutumia fursa hii kuwasihi wananchi wa mkoa wa Pwani na watanzania kwa ujumla kuwa wazalendo kwa nchi yetu kwa kuwafichua watakaojihusisha na vitendo vya Rushwa kuelekea uchaguzi mkuu ujao ili kupata viongozi sahihi wenye nia ya dhati ya kumkomboa Mtanzania.
Aidha, niwasihi watanzania kutoa taarifa zote za vitendo vya Rushwa ikiwemo Rushwa ya Ngono TAKUKURU kupitia namba za BURE 113 AU kwa ujumbe mfupi wa maneno kwa kupiga *113# kisha fuata maelekezo au kutumia TAKUKURU App ili kuongeza tija ya mapambano dhidi ya Rushwa.
Asanteni kwa kunisikiliza, Imetolewa na:
Sadiki Nombo
KAIMU MKUU WA TAKUKURU (M) PWANI

No comments:

Post a Comment

Pages