Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akimpa pole Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al Hafi Hamid alipofika Ubalozi Mdogo wa Nchi hiyo uliopo Migombani kutia Saini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mfalme wa Oman Qaboos Bi Said Al Said.
Balozi Seif Ali Iddi akitia saini Kitabu cha Maombolezo
kwenye Ubalozi wa Oman Zanzibar hapo Migombani kufuatia kifo cha
aliyekuwa Mfalme wa Oman Qaboos Bi Said Al Said.
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al Hafi
Hamid Kushoto akisisitza umuhimu wa Nchi yake kuendelea kuimarisha
Uhusiano wa Kidugu na Zanzibar katika Nyanja tofauti. Picha na – OMPR – ZNZ.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametia saini kitabu cha Maombolezo
kufuatia kifo cha aliyekuwa Mtawala wa
Oman Qaboos Bin Said Al Said kilichotokea Usiku wa kuamkia Jumamosi
iliyopita kwenye Qasri yake ya Beit Al Baraka Nchini Oman.
Marehemu Qaboos Bin
Said Al Said aliyefikisha umri wa Miaka 79 aliitawala Oman kwa miaka 50 ambapo
Utawala wa Nchi hiyo unaoongozwa na Mrithi Mpya Binamu wake Haitham Bin Tariq
aliyekuwa Waziri wa Mirathi na Utamaduni wa Oman ulitenga siku Tatu za
Maombolezo.
Balozi Seif Ali
Iddi alitia Saini Kitabu hicho cha Maombolezo ya Kifo cha Kiongozi huyo wa
Miaka mingi wa Oman kwenye Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Nchi hiyo uliopo Migombani
Mjini Zanzibar.
Akimpa pole
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed
Al Hafi Hamid kufuatia kifo hicho
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kifo cha Kiongozi huyo
kimewagusa Watu wengi wa Visiwa vya Zanzibar na Oman kwa ujumla.
Balozi Seif
alisema Oman na Zanzibar zimekuwa na mafungamano makubwa ya uhusiano wa
Kihistoria wa muda mrefu unaotokana na maingilioano makubwa ya Damu baina ya
Wananchi wa pande hizo mbili.
Makamu wa Pili
wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi wa Oman kuendelea kuwa na moyo wa subra
katika kipindi hichi kigumu cha Msiba kwa kuondokewa na Kiongozi wao
aliyesimamia kuleta mageuzi makubwa ya Kiuchumi ndani ya Taifa hilo la Ghuba.
Akitoa shukrani
zake naye Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al Hafi Hamid alisema Wananchi wa Oman
wamezipokea salamu hizo za Rambi rambi kutoka kwa Ndugu zao wa Zanzibar
akiamini kwamba msiba huo kwa njia moja
au nyengine pia imewagusa Wazanzibari walio wengi.
Dr. Ahmed
alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba licha ya Oman kupata
pengo kubwa la kuondokewa na Kiongozi wao mahiri Marehemu Qaboos lakini bado
Nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuona zile fursa
zilizotolewa hasa katika masuala ya Elimu zinazidi kuimarishwa.
Mfalme Mpya wa
Utawala wa Oman Haitham bin Tariq mbali
ya kuwa Waziri alieshughulikia Masuala ya Mirathi na Utamaduni lakini pia
alikuwa mjumbe wake maalumu wa Marehemu Qaboos katika shughuli muhimu na
aliwahi kufanya kazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman.
Oman
inaendelea kupeperusha Bendera nusu mlingoti kwa muda wa siku 40 kama heshima Maalum
kwa kiongozi huyo wa zamani aliyefariki ambaye ataendelea kukumbukwa na wengi
kwa mchango wake wa kuleta maendeleo na ufanisi mkubwa katika nchi hiyo ya
Kiarabu.
No comments:
Post a Comment