Na Irene Mark
MENEJA wa Huduma za Utabiri kutoka Kituo Kikuu cha Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Samuel Mbuya, ametoa angalizo la mvua, upepo mkali na mawimbi bahari kwa wakazi wa mikoa ya ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi.
Mbuya alitoa angalizo hilo leo Januari 16,2020 na kusema mvua iliyoanza leo itaendelea hadi kesho Januari 17,2020 huku upepo na mawimbi baharini vikitarajiwa kuwepo hadi Januari 21 mwaka huu.
Aliitaja mikoa ambayo baadhi ya maeneo yake yanaendelea kupata mvua ni Dar es Salaam, Pwani, Mtwara na Lindi hivyo kushauri wakazi wa maeneo tajwa kuchukua tahadhari.
"Kwa sababu hiyo tunatarajia maeneo mengi kuathirika kwa sababu ya hizi mvua lakini pia shughuli za uvuvi, usafiri na usafirishaji bahari zinaweza kuathirika pia.
"...Ni vema kila sekta ikazungatia angalizo hili ili kuepusha madhara na wananchi tunawashauri wafike kwenye maeneo yao ya kazi na huduma mapema kuondokana na adha ya uchelewaji njiani," alisisitiza Mbuya.
TMA hutoa huduma ya utabiri kwa kifurushi cha siku tano mfululizo ili kuwarahisishia watumiaji wa taarifa za hali ya hewa kuchukua tahadhari mapema.
No comments:
Post a Comment