HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 01, 2020

TUWAJALI WATU WENYE ULEMAVU: DKT. BASHIRU

Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally.
 

Na Lydia Lugakila, Kagera
 
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt. Bashiru Ally, ameiasa jamii kuwajali na kuwapenda zaidi watu ambao kwa maumbile yao hawawezi kumudu baadhi ya majukumu bila kupata msaada (walemavu), lakini kwa vipawa vyao wanaweza kuisadia jamii na taifa kwa ujumla.

Ameyasema hayo Desemba 30, 2019 alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa makazi ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Mh. Amon Mpanju kijijini kwake Nyakibimbili Bukoba Vijijini.

“Inatakiwa tuwapende zaidi watu ambao kwa maumbile yao, hawawezi kutenda baadhi ya mambo bila msaada, lakini wanavipawa vya kusaidia jamii yao na nchi kwa ujumla, Amoni ni miongoni mwa watu wanaotusikia lakini hawatuoni, ila ninamfaham vema, ni miongoni mwa vijana wachapa kazi zaidi hata ya wanaoona na haya majukumu aliyonayo hajapewa kwa sababu haoni ila ni kwa kuwa anauwezo wa kuyamudu sawasawa”.

Dkt. Bashiru ameongeza kuwa, tuendelee kuwapenda watoto na mapenzi makubwa ni namna ya kuwandaa kupata elimu, Amoni amefika hapo alipo kwa kuwa hao waliompenda walifanya kazi ya kumuelimisha licha ya changamoto zote, na katika hili nipende kuwapongeza walimu nchi nzima kwa kazi mnayoifanya ambayo ni kazi ya kitakatifu, ni kazi ya ukombozi na leo mmemkomboa Amoni mpaka hapa alipofika na ninawaomba sana muendelee kukomboa wengine ili tuwapate wakina Amoni wengi.

Awali akimkaribisha Katibu Mkuu, Mhe. Mpanju alianza kwa kushukuru ujamaa kwa kuwa anaamini bila ujamaa yeye leo asingekuwepo kwani alifiwa na wazazi wote akiwa na umri mdogo sana, ila alilelewa na watu wengi na wengine hata asiowajua kwa sababu ya uwepo wa ujamaa na undugu miongoni mwa watanzania.

“Nimepita mawimbi mazito katika maisha yangu, mengine hayaelezeki kirahisi, nilifiwa na wazazi wangu wote wawili nikiwa na umri mdogo sana mwaka 1992 nyumbani hatukuwa na uwezo kabisa, ujamaa ndio ulionisaidia kuishi, kwa kuwa nililelewa na watu wengi hata wengine nisiowajua  akiwemo mama Selina, mama Sevelin na wengine wengi, ninawapenda sana, walinifuta machozi”.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa nyumba yake haukuwa mwepesi, alianza tangu mwaka 2007 na alinunua kiwanja hiko kwa fedha ya kujikimu (boom) alipokuwa chuo kikuu cha Dar Es Salaam, aliendendelea kuweka fedha kidogo kidogo mwaka 2010 aliposhiriki kampeni ya uchaguzi mkuu, aliposhiriki bunge la katiba, Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na sasa ni miaka kumi na miwili nyumba imesimama, hivyo nyumba hii itakuwa ni ya jamii nzima na si yangu pekee.

Viongozi mbalimbali wa dini wakitoa nasaha zao, akiwemo Shekhe wa Mkoa wa Kagera Bw. Haruna Kichwabuta alisema, moja ya maagizo ya mwenyezi Mungu baada ya kuwa mtu mzima, ni kuwa na vitu vitatu ambavyo ni Mwenza/Mke, Makazi na Usafiri ambavyo vyote vipo kwa sababu, hivyo leo ni siku ya furaha kwa kijana wetu kutimiza moja ya matakwa ya mwenyezimungu ambayo ni kuwa na makazi, vijana wote tuige mfano huu mwema hapa Duniani na mbinguni.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Bukoba Mhe. Deodatus Kinawiro, viongozi wa Chama mkoa na wilaya, viongozi wa dini, wenyeviti mbalimbali wa vijiji na wananchi.

Katibu Mkuu yupo Wilayani Bukoba kwa mapumziko ya siku kumi ambapo anatarajiwa kumaliza mapumziko hayo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020.

No comments:

Post a Comment

Pages