HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

December 31, 2019

KANISA LA AIC LAHIMIZA AMANI, KUWATUNZA WAJANE

Waumini wakiwa kanisani kumwabudu Mwenyezi Mungu.


Na Sitta Tumma, Magu

KANISA la African Inland Church (AIC) Dayosisi ya Mwanza, limewataka viongozi na vyombo vya dola nchini, kuhakikisha wanailinda amani ya nchi kwa kutenda haki.

Aidha, limeshauri Watanzania kuwasaidia wanawake wajane katika changamoto zinazowakabili, kwani ni agizo la Mwenyezi Mungu.

Kauli hiyo imetolewa na Askofu Mkuu mstafu wa Dayosisi hiyo, Daniel Nungwana, wakati wa Misa Takatifu iliyofanyika Kanisa la AIC Isangijo, Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza, Jumapili kuelekea mwaka mpya 2020.

Alitaka kila mtu bila kujali jinsia, rika na cheo chake kulinda amani ya nchi, akisema amani ni tunda la haki.

"Wakitokea wakimbizi siyo kwamba wafadhili watatuletea amani. Watatusaidia kuleta misaada blanketi, mahema na kila kitu, lakinihawatatununulia amani.

"Kwa hiyo, amani lazima tuitunze sisi wenyewe. Na wa kuitunza amani ndiyo sisi wasimamizi wa amani," alisema Askofu Nungwana wakati akihubiri kanisani hapo.

Kwa mujibu wa Askofu Nungwana, punde amani inapoteteleka taifa huyumba wakiwamo wanawake na watoto hupata tabu ya maisha na mahitaji muhimu.

Katika misa hiyo, ulitolewa msisitizo na kanisa hilo kwa Watanzania kuwajali na kuwasaidia wanawake wajane, ili kukidhi mahitaji yao.

Ilielezwa kuwa, wajane wengi wanakabiliwa na changamoto za mahitaji mbalimbali, hivyo usaidizi dhidi yao unahitajika ikiwa ni pamoja na kuwapa misaada mbalimbali ya kibinadamu.


ASKOFU MAFUJA

Askofu wa AIC Dayosisi ya Mwanza, Philip Mafuja, alisema wajane ni watu muhimu katika maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla, hivyo wanahitaji kupewa ushirikiano na wanadamu.

"Katika kitabu cha Wafalme wa Pili Sura ya nne tuliyosoma, tunamuona mtumishi wa Mungu Nabii Elisha, akionesha na kuthibitisha uwezo wa mungu kwa muhitaji huyu ambaye alikuwa mama mjane.

"Kwa maana hiyo, tunao wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha tunapendana na kuthaminiana. Tumsaidie huyu mama mjane," alisema Askofu Mafuja wa Kanisa la AIC Dayosisi ya Mwanza.

Katiba Misa hiyo, wajane takribani 15 walipewa misaada mbalimbali zikiwamo nguo, sabuni na mahitaji mengine kadri yalivyopatikana kutoka kwa jamii na washirika wengine.

         MCH GOMUGO ANENA

Kwa upande wake, Mchungaji wa Kanisa hilo la AIC Isangijo, Wilaya ya Magu Mkoa wa Mwanza, Isack Gomugo, alihimiza kumtegemeza kwa misaada mbalimbali mama mjane.

Alisema kanisa hilo limejiwekea utaratibu wa kuisaidia jamii hiyo kukabiliana na changamoto zinazowaegemea, ambapo huwapatia vitu mbalimbali kwa ajili ya familia zao.

"Tunapokuwa tunakutana angalau tupate uwezo wa kumsapoti mjane mmoja au wawili au watatu.

"Hilo tumelitambua na tukaona kwamba ni jema. Kwa hiyo tunatamani tuliombee na tulitekeleze," alisema Mchungaji Gomugo mbele ya waumini kanisani hapo Isangijo.

Kulingana na Kanisa hilo la AIC, japo Mungu anaagiza wajane na watu wote kupendana, lakini ni jambo muhimu zaidi jamii kutenda mambo mema yanayompendeza Masiha.

Mchungaji Gomugo mbali na kuiomba jamii kupendana, alisema kanisa linaufanyia kazi ushauri wa kuwakatia bima za afya wanawake wajane.

"Suala la bima ya afya kwa mjane ni muhimu sana," alisisitiza Gomgo huku akiwasihi Watanzania kujitenga na matendo maovu ya ulimwengu.

No comments:

Post a Comment

Pages