HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

January 31, 2020

Waandishi Washauriwa Kuelimisha Jamii dhidi ya NCD

 Mtalaam wa mazoezi, Waziri Ndonde, akitoa elimu kwa waandishi wa habari wakati wa semina ya mafunzo hayo.
 Mtaalam wa Chakula na Lishe, Marry Materu, akizungumzia wakati wa mafunzo hayo kuhusu namna bora ya ulaji wa vyakula ili kuepuka magonjwa yasiyoyakuambukiza mwilini.
 Mkurugenzi wa Jukwaa la kudhibiti matumizi ya tumbaku nchini, Lutgard Kagaruki, akiwa kwenye semina hiyo kabla ya kuanza kutoa mada kuhusu madhara ya tumbaku wakati wa mafunzo hayo.
 Profesa Andrew Swai, akitoa mada wakati wa mafunzo hayo kwa waandishi wa habari yaliyolenga kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazohusu magonjwa yasiyoyakuambukiza.
Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia mada mbalimbali wakati wa semina ya mafunzo yanayohusu kuandika habari za magonjwa yasiyoyakuambukiza. Mafunzo hayo yamefanyika leo Januari 31 mwaka 2020 jijini Dar es Salaam.
 Meneja Mradi kutoka Shirikisho la Vyama vya Magonjwa yasiyoyakuambukiza, Happy Nchimbi, akisikiliza kwa makini bada zilizokuwa zinatolewa na watalaam mbalimbali wakati wa mafunzo hayo.

 
Na Suleiman Msuya
WAANDISHI wa habari nchini wameshauriwa kuandika kwa kina habari za Magonjwa Yasiyoambukiza (NCD), ili jamii iweze kuelimika na kukabiliana nayo.
Ushauri huo umetolewa na Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Magonjwa Yasiyoambukiza (TANCDA), Profesa Andrew Swai wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari zinazohusu magonjwa yasiyoambukiza.
Prof. Swai alisema magonjwa yasiyoambukiza yanaweza kupatiwa ufumbuzi iwapo jamii itapatiwa elimu ya namna ya kuisha hasa katika matumizi ya vyakula.
“Kuna magonjwa yasiyoyakuambukiza na yanamaliza watu ukifuatilia kwa kina unaona sababu kubwa ni mfumo wa maisha ambao tunaishi sasa,” alisema.
Alisema watu sahihi wa kuelimisha jamii kuhusu mfumo wa maisha ni waandishi wa habari hivyo ni jukumu lenu kutumia kalamu zenu kufikisha ujumbe sahihi kuhusu magonjwa hayo ambayo yanapoteza maisha ya watu wengi duniani.
Mwenyekiti huyo alisema magonjwa kama kisukari, saratani, shinikizo la damu na mengine yanaweza kupatiwa majibu sahihi iwapo jamii itaelimika mapema.
“Mimi nimegundulika kuwa nina kisukari lakini kwa sababu ya kuzingatia mambo muhimu kuanzia aina ya maisha, vyakula na mazoezi hainitesi ninaweza kusema sina kwa sababu vyote ambavyo wasio na kisukari wanakula na mimi nakula,” alisema.
Kwa upande wake Meneja Mradi wa TACDA, Happy Nchimbi alisema shirikisho hilo limejipanga kushirikiana na waandishi wa habari kama kiungo muhimu cha kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu magonjwa hayo.
“Lengo la kutoa mafunzo haya ni kuwajengea uwezo wa kuandika habari zinazohusu magonjwa hayo ili kuhakikisha jamii ya Watanzania inapata taarifa sahihi.
Nchimbi alisisitiza kuwa msingi mkubwa wa kutoa mafunzo hayo ni kuhakikisha waandishi wanauelewa wa kutosha kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na visababishi nyake.
Alifafanua shirikisho hilo lenyewe haliwezi kufikisha taarifa hizo kwa wananchi na kwamba bila kutumia waandishi wa habari ambao wana uwezo wa kufikia wanachi wote katika ngazi zote wenye vipato na wasio na vipato, wa mijini na vijijini.
Aliongeza kuwa matarajio yao baada ya mafunzo hayo waandishi watakuwa na uelewa wa kutosha kuhusu magonjwa yasiyoambukiza na kwenda kutoa elimu hiyo kwa jamii.
"Ni matarajio yetu elimu ambayo itatolewa itasaidia wananchi wengi ambao hawana elimu ya kutosha juu ya magonjwa haya kuipata,"amesema.
Alisisitiza kuwa magonjwa yasiyoambukiza yapo na yanakuwa kwa kasi ambapo utafiti wa mwaka 2012  ilionesha asilimia 9 ya wananchi wanaishi na ugonjwa wa kisukari na asilimia 26 ina shinikizo la juu la damu, lakini pia viwango vya ufanyaji mazoezi viko chini ulaji wa matunda na mboga za majani ni mdogo sana.
Meneja huyo alisema magonjwa hayo yanapoteza maisha ya wananchi wengi, hivyo ameshauri jamii ya Watanzania kujiepusha kwa kuzingatia mlo ulio sahihi ambao una viwango vidogo vya sukari, chumvi na mafuta.

No comments:

Post a Comment

Pages