Katibu wa Kamati ya Uadilifu Chama cha ACT - Wazalendo, Maalim Abubakar Khamis Bakar, akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ndogo ya chama hicho kuhusu ugawaji wa vitambulisho vya Mzanzibar mkaazi unaoendelea kisiwani Pemba. (Picha na Talib Ussi).
Na Talib Ussi, Zanzibar
Wananchi 9,000 katika Wilaya ya Micheweni Mkoa wa Kaskazini
Pemba hawajapata vitambulisho vyao vya Mzanzibari Mkaazi, wakati zoezi
hilo limemalizika katika wilaya hiyo na kuendelea katika wilaya ya Chake
Chake.
Akizungumza na waandishi wa habari Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha ACT - Wazalendo, Hamadi Mussa Yusuf, amesema Idara ya Usajili wa Matukio ya Kijamii haijatoa ratiba rasmi ya uchukuaji wa vitambulisho hivyo hutolewa bila ya taarifa ni wajibu wao kuweka ratiba hiyo.
‘Tunataka Idara ya usajili na matukio ya kijamii kuhakikisha wananchi elfu tisa kutoka Wilaya ya Micheweni wanaotaka kujiandikisha katika daftari la wapiga kura ifikapo tarehe 18 January mwaka huu wawe wameshapata vitambulisho vyao kabla ya tume ya uchaguzi haijaanza zoezi la kuandikisha”alisema Hamadi Mussa.
Hivyo wameitaka Tume ya Uchaguzi ZEC kuandaa maazingira mazuri na kuhakikisha watu wamepata vitambulisho vya mzanzibari mkaazi kabla ya kuandikisha daftari la wapiga kura.
Alisema mtu yeyote hawezi kuandikwa katika daftari la wapiga kura mpaka aoneshe kitambulisho chake cha Mzanzibari mkaazi hivyo kumkosesha kitambulisho ni kumnyima haki yake ya msingi.
“Pamoja na kuwa hawafanyi kazi kwa pamoja Tume ya Uchaguzi na Idara ya usajili wa matukio ya kijamii lakini tunaitaka tume ya uchaguzi kujiridhisha kwanza kama wananchi wamepatiwa vitambulisho kabla ya wao kuanza kuandikisha kwenye daftari.”alisema Hamad Mussa.
kwa upande wake Katibu wa Kamati ya Uadilifu wa Chama cha ACT - Wazalendo ambaye pia Mwanasheria na Waziri mstaafu wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakari, alisema kwa mujibu wa sharia No 7 ya mwaka 2005 kila Mzanzibari ana haki ya kupata kitambulisho na kama unamnyima ni kosa.
Alisema idara ya usajili na matukio ya kijamii imekuwa ikiwahangaisha watu wanaotaka kupatiwa vitambulisho vyao kwa kutembea masafa marefu na unapofika katika ofisi yao unaambiwa kitambulisho hakipo urudie siku nyengine.
Alisema unyanyasaji huo wanafanyiwa watu kwa lengo la kuwavunja moyo ili kuwakosesha vitambulisho hivyo na kuwanyima haki ya kujiandikisha katika daftari la wapiga kura.
Aidha Mwansheria Abubakar alisema hata utendaji wa wafanyikazi wa vitambulisho unamtia mashaka kwani hawana uelewa wa kutoka katika kazi zao wanazozifanya na kusababisha usumbufu mkubwa wakati wa kumtafutia mtu kitambulisho chake.
Hata hivyo amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kudai haki yao ya kupata kitambulisho.
No comments:
Post a Comment