Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipofunga Mkutano wa
Kimataifa wa Uwekezaji Katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020
kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere
jijini Dar es Salaam, Februari 23, 2020.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuzindua Utoaji wa Cheti cha
Uhalisia kwa Madini ya Bati kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akionesha cheti cha uhalisia wa Madini ya Bati baada ya uzinduzi uliofanyika jijini Dar es Salaam. Kulia ni Spika wa Bunge, Job Ndugai, Waziri wa Madini, Doto Biteko (wa pili kushoto) na Waziri wa Nchi Anayeshughulikia Maendeleo ya Madini wa Uganda, Sarah Opendi (kushoto). (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema hatua iliyofikiwa
ya kuzuia uvunaji haramu wa rasilimali kwa utaoji wa cheti cha uhalisia
kwa madini ya bati, kutaiwezesha sekta ya madini nchini kuchangia
kwenye pato la Taifa kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2025.
Ameyasema
hayo leo (Jumapili, Februari 23, 2020) wakati wa kufunga Mkutano wa
Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania wa mwaka 2020 kwa
niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli. Mkutano huo wa siku mbili
ulifanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere.
Waziri Mkuu ambaye amezindua utoaji wa cheti cha uhalisia (certificate of origin) kwa
madini ya bati kitakachokuwa kinatolewa na Tanzania, amesema cheti
hicho ni muhimu kwa Taifa letu na nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maziwa
Makuu kwa kuwa kitaweka utaratibu wa kudhibiti madini hayo.
Waziri
Mkuu amesema mambo waliyojifunza katika mkutano huo yatasaidia kuongeza
kasi ya kukua kwa mchango wa sekta ya madini katika pato la Taifa.
“Wizara ya Madini shirikianeni na wadau wengine katika kuhakikisha
mkutano huu unaendelea kuboreshwa kila mwaka na kuongeza washiriki ili
kupanua uelewa wa pamoja.”
Waziri
Mkuu amesema kuwa ni matarajio ya kila mmoja wao kwamba uzinduzi huo
walioufanya utasaidia katika kutekeleza Itifaki ya Kuzuia Uvunaji Haramu
wa Rasilimali yaani ‘Protocol Against the Illegal Exploitation of Natural Resources’
“…nafahamu
kwamba mkutano wa aina hii unaoihusu sekta ya madini unafanyika kwa
mara ya pili hapa nchini. Nitoe wito kwa nchi wananchama kuhakikisha
mikutano ya aina hii iweze kuandaliwa katika nchi nyingine na iwe
endelevu katika kutoa fursa kwa wadau kutambua fursa zilizopo nchi
nyingine.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali inaridhishwa na kuimarika kwa utendaji kazi wa
sekta ya madini nchini kutokana na mafanikio yake ikiwemo kuongezeka kwa
mchango wake katika pato la Taifa. “Mathalan, kupitia Taarifa ya Hali
ya uchumi ya Mwaka 2019, katika kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka wa
fedha 2019/2020, mchango wa Sekta ya Madini ulikua kwa asilimia 13.7.”
Waziri
Mkuu amesema kwenye kipindi hicho, sekta ya madini ilikuwa ya pili
katika kuchangia pato la Taifa ikitanguliwa na sekta ya ujenzi ambayo
ilichangia pato la Taifa kwa asilimia 16.5.
“Katika
kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2019/2020, Serikali kupitia sekta ya
madini imeweza kukusanya sh. bilioni 242.53 sawa na asilimia 51.5 ya
lengo la mwaka la kukusanya sh. bilioni 470.89.Makusanyo hayo yalitokana
na mrabaha, ada ya ukaguzi wa madini, huduma za kimaabara, mauzo ya
machapisho mbalimbali ya kijiolojia na ada za leseni.”
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amesema katika kukabiliana na utoroshwaji wa madini,
Serikali iliamua kuanzisha masoko ya madini nchini kwa lengo la kuondoa
mianya ya kuweza kufanya biashara ya madini kupitia njia zisizo rasmi.
“Hadi sasa tuna jumla ya masoko ya madini 27 na vituo vidogo vya ununuzi
wa madini 28 kote nchini.”
Amesema
masoko hayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha upatikanaji
sahihi wa takwimu za madini tofauti na ilivyokuwa awali kabla ya
kuanzishwa kwake, hivyo ametumia fursa hiyo kuwafahamisha wadau wa
mkutano huo kuwa masoko hayo yapo wazi kwa wadau wa ndani na nje ya
nchi.
Waziri
Mkuu ametoa wito kwa nchi ambazo bado hazijaanzisha masoko ya madini
kutumia masoko yaliyoko nchini wakati wakijipanga kuanzisha masoko yao.
“Masoko
haya yanafanya kazi katika misingi ya kiushindani na uwazi wa
kibiashara. Pia, niwahakikishie kuwa masoko yetu yana ulinzi na usalama
wa kutosha na sifa zote za kimataifa zinazohitajika katika kuendesha
biashara hiyo. Hivyo, yatumieni vizuri masoko haya.”
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa sambamba na kuanzishwa kwa masoko ya madini,
Serikali pia imefanikiwa kuhamasisha wamiliki wa migodi kuchangia zaidi
katika huduma za jamii nakuimarisha usimamizi wa shughuli zinazofanywa
na wachimbaji wakubwa, wa kati na wadogo wa madini.
“Vilevile,
Serikali imefanikiwa kuongeza ushiriki wa moja kwa moja wa Serikali
katika kumiliki na kusimamia migodi, ikiwa ni pamoja na kumilikishwa
asilimia 16 ya hisa katika migodi;na kufungamanisha sekta ya madini na
sekta nyingine za uchumi.”
Awali, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano huo umehudhuriwa na nchi 11 wanachama waJumuiya ya Nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) pamoja na wadau wa sekta ya madini wa ndani na nje ya nchi.
Waziri
Biteko alisema lengo la mkutano huo ni kuwakutanisha wadau wa madini
katika nyanja tofauti tofauti ikiwemo wachimbaji, wanaotengeneza na
kuuza tekinolojia, wadau wenye mitaji na wasionayo lakini pia kwa upande
wa Serikali kujifunza namna ya kuboresha na kuifanya sekta ya madini
kuwa ni sekta yenye kuongeza tija kwa Taifa.
No comments:
Post a Comment