Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa, akimkabidhi
kitabu Kaimu Mkurugenzi wa Benki ya NMB- Ruth Zaipuna wakati wa hafla
ya kutambulisha na kutia saini kitabu chake iliyofanyika jijini
Mwanza.
Kaimu
Mkurugenzi wa Benki ya NMB - Ruth Zaipuna akitoa mada kuhusu
ubinafsishaji wa benki hiyo wakati wakati wa hafla ya utambulisho wa
kitabu cha
"My Life, My Purpose" kilichoandikwa na Mhe. Benjamin Mkapa, Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu Mhe. Benjamin Mkapa katika picha ya pamoja na uongozi wa Benki ya NMB.
Na Mwandishi Wetu
Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Benjamin Mkapa amesifu uamuzi wa Serikali yake kwa kuamua
kuibinafsisha Benki ya NMB.
Akizungumza jijini Mwanza juzi wakati wa hafla ya kutambulisha
kitabu chake cha: My Life, My Purpose – (Maisha Yangu, Dhamira Yangu), Rais
huyo Mstaafu alisema suala la ubinafsishaji taasisi hiyo ulitokana na uamuzi wa
mwanzoni mwa utawala wake mara baada ya kuingia madarakani mwaka 1995.
Ilipofika mwaka 1997, Serikali ya Rais Mkapa iliamua kuundwa kwa
Benki ya NMB baada ya kugawanywa kwa iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara
(NBC).
Baada ya kuundwa kwa NMB mwaka 1997, mwaka 2005 serikali ya Rais
Mkapa iliuza asilimia 49 ya hisa za NMB kwa wawekezaji wa Rabobank ya Uholanzi.
“Nafarijika kuona NMB ni
miongoni mwa mabenki makubwa yenye mtandao mkubwa nchini ikihudumia wananchi wa
kawaida hadi vijijini,” alisema Mkapa
Akionyesha
kuchukizwa na wanaokosoa uamuzi wa ubinafsishaji uliochukuliwa na serikali
yake, Rais Mkapa alisema watu wanatakiwa kuelewa kuwa wakati huo ilikuwa ni
lazima kufanya uamuzi ili kuokoa pesa za walipakodi zilizokuwa zikipotea kwa
kutolewa kama ruzuku ya kuendeshea mashirika ya umma.
Ndani
ya kitabu chake, kuna aya inayosema wanaokosoa uamuzi wa ubinafsishaji
wanapaswa kuelewa kuwa wakati huo, mashirika ya umma yalikuwa na hali mbaya
kifedha kiasi kwamba serikali ililazimika kutumia kiasi kikubwa cha pesa za
walipakodi kugharamia uendeshaji wa mashirika hayo. “…hiyo siyo kazi moja wapo
ya pesa za serikali,” anaandika Mkapa.
Akizungumzia mafanikio ya benki hiyo, Kaimu Mkurgenzi Mtendaji
wa NMB, Ruth Zaipuna alisema kwa kipindi cha miaka 22 iliyopita, benki hiyo
imejipambanua kuwa mfano bora wa uamuzi wa ubinafsishaji baada ya kufikia kuwa kimbilio
la wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa kwa mitaji na ushauri wa kitaalam.
Kwa
miaka 22 ya uwepo wake, Benki ya NMB imetoa jumla ya Shilingi trillioni 1.2
kusaidia biashara ndogo na za kati na mikopo mingine Shilingi trilioni 2.2
kusaidia wateja binafsi.
Katika
kusaidia wakulima, Bi. Zaipuna alisema mwaka huu wa 2020, Benki imepanga
kufungua akaunti zaidi ya 300,000 za wakulima ili kuhakikisha kuwa wakulima
wanapata malipo yao kupitia mfumo rasmi wa fedha na hivyo kuchangia katika
kukuza huduma jumuishi za fedha (financial inclusion) hapa nchini.
Bi.
Zaipuna alisema Benki ya NMB imeendeleza ushirikiano wake na Mfumo wa Kielektroniki wa
Malipo ya Serikali (Government's electronic payment system – GePG),
ambapo mpaka hivi sasa taasisi 590 za serikali zimeunganishwa katika mfumo huo.
Kupitia mfumo wa GePG, Benki ya NMB huwezesha kukusanya kwa jumla ya mapato ya
serikali yapatayo Shilingi trilioni 2.1.
“Tunafanya
hivyo kwa kutambua kuwa ni wajibu wetu kuunga mkono miradi ya kimkakati ya
serikali. NMB ndiyo iliyokuwa benki ya kwanza kuunganishwa na mfumo wa GePG,”
alisema.
No comments:
Post a Comment