MKURUGENZI wa Taasisi
ya The Society Awareness, Felix Makuwa,
amesema kauli za viongozi wa vyama vya siasa na wastaafu kudai Katiba mpya na
Tume Huru ya Uchaguzi wakati huu hazina afya kwa maendeleo ya nchi kwa sasa.
Makuwa ametoa kauli
hiyo kwenye taarifa aliyoitoa jana jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari
yenye kichwa cha habari kinachosema ‘Uhusiano tata ya Mheshimiwa Jaji Joseph
Sinde Warioba na upinzani (Ukawa)
Mkurugenzi huyo alianza
kwa kuwatahadharisha Watanzania wawe macho kuhusu kauli tata zinazozuka sasa
wakati huu ambao nchi inajiandaa na uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani.
Makuwa ambaye
alijitambulisha kuwa ni mwanaharakati alisema kwa siku za karibuni baadhi ya
watu wamekuwa wakitumia majukwaa kudai katiba na tume huru jambo ambalo
linaibua maswali mengi.
Alisema katika kilele
cha miaka 58 ya uhuru jijini Mwanza, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Freeman Mbowe alizungumzia suala la maridhianbo ya kisiasa na baadae
akamuandikia barua Raisi kulalamikia mambo mbalimbali.
“Baadhi ya mambo hayo
ni tume huru ya uchaguzi huku wakijua kuwa tume zote mbili (NEC) na (ZEC) ni
huru na ndio maana ndani ya Bunge kuna wabunge wa upinzani.
Nimeshangazwa mda sio
mfupi baada ya barua hiyo ya Chadema
kwenda kwa Rais, ameibuka aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Katiba Jaji mstaafu
Warioba na kuzungumzia hitaji la katiba mpya.
Makuwa alisema Warioba
alisimamia mchakato wa Katiba ambayo ilikwama hivyo hana sababu ya kuanzisha
habari za Katiba mpya kwa kuwa Katiba iliyopo inakidhi vigezo kwa kusimamia
haki na amani tangu kupatikana kwa uhuru.
Mwanaharakati huyo
alihoji maswali iwapo tume hakuna wabunge wamepatikanaje ni kwanini sasa ndio
wanaibuka wanaodai tume huru na kwanini sasa yanaonekana mahusiano ya watu wa
Chadema na CCM kudai kitu kimoja.
Alitolea mfano kuwa
Warioba alipewa nafasi katika tume hio
na akazalisha rasimu ambayo ililenga kuvunja amani ya nchi kama serikali haingekuwa makini,
ingawa rasimu hiyo ilikuwa rafiki wa wapinzni.
“Hivi jamani kama kuna jambo
zuri linalohusu Katiba, kiongozi mkuu kama Warioba aliona shida gani kwenda
kumuona Rais John Magufuli na kumshauri bila kukimbilia vyombo vya habari na
pia huu ujasiri kuiyelekeza nchi kupitia vyombo vya habari unatoka wapi?.
Mwanaharakati huyo
amewaomba na kuwaasa Watanzania wawe macho na wajihadhari na watu hawa ambao wapo tayari kupindisha ukweli na amani
ya nchi kwa kisingizio cha Katiba mpya
au tume huru ya uchaguzi.
Makuwa alisema tume
huru au katiba mpya sio muarubaini wakupata viongozi bora au wachapa kazi bora.
Aidha alimshauri
Msajili wa Vyama vya Siasa kuchukua hatua dhidi ya vyama na wanasiasa ambao
amedai wanapotosha umma kwa maslahi yao.
No comments:
Post a Comment