HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 13, 2020

TMA yatabiri mafuriko mvua za masika

 
 
 
Na Irene Mark
 
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Dk. Agnes Kijazi amesema mwaka huu mvua za masika zitaanza wiki ya pili ya Machi hadi mwishoni mwa Mei mwaka huu, huku zikitarajiwa kuwa juu ya wastani.
Mvua hizo zitanyesha kwenye mikoa ya Kaskazini Mashariki ya nchi ambayo ni Manyara, Kilimanjaro na Arusha.
Dk. Kijazi alisema hayo Dar es Salaam alipotangaza utabiri wa msimu wa mvua za masika mbele ya waandishi wa habari na kuongeza kwamba mvua za nje ya msimu zitaendelea hasa kwa maeneo ya Pwani ya Kaskazini yenye mikoa ya Tanga, Dar es Salaam, Pwani, visiwa vya Unguja na Pemba na Kaskazini mwa Morogoro.
Kwa mujibu wa taarifa za TMA mvua za masika mwaka huu zinafanana na zilizonyeesha mwaka 2007 hivyo kuwataka wananchi kuchukua tahadhari ya mafuriko na maafa mengine yatokanayo na mvua.
Alisema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, hali ya joto juu la wastani itaendelea kuwepo mpaka masika yatakapoanza.
"Maeneo ya Pwani ya Kaskazini mikoa ya Dar es Salaam, ikijumuisha kisiwa cha Mafia , Tanga na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro pamoja na  visiwa vya Unguja na Pemba... ukanda wa Ziwa Victoria katika Mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu na Mara  pamoja na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.  
"Kutokana na mifumo ya hali ya hewa ilivyo kwa sasa na inavyotarajiwa kuwa kwa kipindi chote cha msimu huu kwa ujumla mvua za wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua kwa mwaka.
"Hata hivyo, maeneo mengi ya nyanda za juu Kaskazini Mashariki, Mashariki na Kusini mwa Ziwa Viktoria, mkoa wa Tanga na visiwa vya Unguja na Pemba yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani kipindi cha masika.  
"...Upande wa Magharibi mwa Ziwa Viktoria na maeneo mengine ya Pwani ya Kaskazini  mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikijumuisha kisiwa cha Mafia na maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Morogoro yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi chini ya wastani," alisema Dk. Kijazi
Kutokana na hali hiyo ,TMA imewashauri wadau wa sekta mbalimbali  ikiwemo Kilimo na Usalama wa Chakula, Mifugo na Wanyamapori, Maliasili na Utalii, Nishati na Maji, Miji, Afya na Menejimenti za Maafa kujipanga kukabiliana na majanga.
Alisema hali ya mafuriko inaweza kusababusha milipuko ya magonjwa na wadudu waharibifu kujitokeza kutokana na unyevunyevu na kutuama kwa maji. 
Mkurugenzi huyo alisema uwepo wa mvua za kutosha, utaongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali na malisho ya mifugo na wanyamapori. 
Alisema mvua za Msimu zilizoanza Novemba, mwaka jana  katika maeneo yanayopata msimu mmoja wa mvua kwa mwaka, mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora, Katavi, Kigoma, Rukwa, Mbeya, Songwe, Njombe, Iringa, Ruvuma, Lindi, Mtwara na Kusini mwa mkoa wa Morogoro zinaendelea vizuri kama ilivyotabiriwa.
"Tutaendelea kutoa taarifa za mrejeo kila itakapowezekana hivyo tunaomba muieleze jamii kwamba wazingatie zaidi tarifa za mrejeo zinazotoka kila saa24 na vifurushi vya siku tano," alisisitiza Dk. Kijazi.

No comments:

Post a Comment

Pages