Badhi ya miili ikishushwa kwa ajili ya kutoa nafasi kwa ndugu jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho.
Badhi ya miili ikishushwa kwa ajili ya kutoa nafasi kwa ndugu jamaa na marafiki kutoa heshima za mwisho.
Majeneza ya miili ya watu waliofariki katika tukio la kugombea mafuta ya upako.
Baadhi ya ndugu wakilia kwa uchungu wakati miili ikiwasili kwenye Uwanja wa Mashujaa mjini Moshi.
Simanzi yatanda kuagwa waliokufa kwa Mwamposa
>>>Viongozi wa dini wamtupia lawama Mwamposa
NA JABIR JOHNSON, MOSHI
Simanzi
imetanda katika tukio la kuagwa kwa miili ya watu waliofariki wakati
wakihudhuria ibada katika Kanisa la Inuka na Uangaze Februari Mosi mwaka
huu linaloongozwa na Mtume na Nabii Boniface Mwamposa maarufu
Bulldozer.
Tukio
hilo la kuagwa kwa miili ya marehemu hao limefanyika katika viwanja vya
Mashujaa mjini Moshi, Kilimanjaro Februari 3 mwaka huu na kuhudhuriwa
na watu kutoka viunga mbalimbali mkoani humo.
Miili
ya watu 20 waliopoteza maisha wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto
iliwasili katika viwanja hivyo saa 5: 56 asubuhi ikiwa katika magari ya
Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro aina ya Ashok Leyland PT 4062 na PT
4374.
Baada
ya kufika viwanjani hapo ilipokelewa kwa hisia za huzuni na majonzi
huku wengine wakibubujikwa na machozi wakishindwa kuamini kama ndugu,
jamaa na marafiki wao wakiwa ndani ya majeneza tayari kufanyiwa sala ya
pamoja kisha kukabidhiwa kwa ajili ya utaratibu wa familia.
KAMANDA WA POLISI ATOA TAARIFA YA TUKIO LILIVYOKUWA
Kamishna
Msaidizi wa Jeshi la Polisi (ACP) mkoa wa Kilimanjaro Said Hamduni
alisema Mwamposa aliomba kibali cha siku tatu cha mkutano wake katika
uwanja wa Majengo kuanzia saa 8:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.
Aidha
ACP Hamduni alisema mpaka sasa Jeshi la Polisi limewakamata watu saba
kwa mahojiano zaidi akiwamo Mtume na Nabii wa huduma hiyo ya Inuka na
Uangaze Boniface Mwamposa kuhusiana na tukio hilo na kwamba sheria
itafuata mkondo wake.
Katika tukio hilo watoto waliopoteza maisha ni watano na mwanaume mmoja huku wanawake wakiwa ni 14.
VIONGOZI WA DINI WAMTUPIA LAWAMA MWAMPOSA
Viongozi
wa Dini mbalimbali waliungana katika tukio hilo la kuiaga miili ya
waliopoteza maisha wakiwamo Askofu Glorius Shoo wa Tanzania Assemblies
of God; Mchungaji Andrew Munis wa K.K.K.T; Fr. Colman Siriwa wa Kanisa
la Katoliki na Sheikh Abdallah Mfaume ambaye aliiwakilisha Bakwata.
“Vifo
vinavyotokana na majanga ya asili hivyo hatuwezi kuviepuka, lakini
kilichotokea juzi kinaepukika kimetokea kwa uzembe wetu, na ulaghai
wetu;” alisema Mchungaji Andrew Munisi.
“Tusitumie uhitaji watu kuwa mtaji wetu,…tusitumie Biblia isivyopasa,” alisisitiza Mchungaji Munisi.
“Maswali
ni mazito na ni magumu sana, majibu ni mazito, Bakwata inawaomba wana
kilimanjaro kuwa watulivu wakati wa kuyapata majibu ya suala hilo kwani
hayahitaji majibu mepesi. Tujenge Imani katika mafundisho sahihi,”
alisema Sheikh Abdallah
RC KILIMANJARO AWAASA WANANCHI NA VIONGOZI WA DINI
Mkuu
wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira aliwataka viongozi wa dini kuwa na
utaratibu mzuri wa kusimamia waumini wao katika maeneo yao ya ibada ili
kusitokee tena mkanyagano ambao utaweza kuathiri maisha ya watu.
Aidha
Dkt. Mghwira aliongeza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
John Pombe Magufuli alimpigia simu na kumtaka kuwa asifunge huduma hiyo
ya Inuka na Uangaze na kwamba utaratibu wa ibada uendelee kama kawaida.
No comments:
Post a Comment