HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 11, 2020

TATIZO LA MAJI WILAYANI UYUI KUENDELEA KUPATIWA UFUMBUZI-RUWASA

Na Tiganya Vincent
  
SERIKALI imeanza zoezi la kuwaondolea tatizo sugu la maji wakazi wa Wilaya ya Uyui baada ya kuanza utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kupeleka maji katika maeneo mbalimbali ya eneo hilo.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Meneja wa Wakala wa Maji safi na usafi wa mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Uyui Godfrey Shibiti wakati akiwasilisha mpango wa kutatua maji katika eneo hilo wakati wa kikao cha Baraza la Maadiwani.

Alisema Serikali katika awamu ya kwanza imetoa shilingi milioni 100 kwa ajili ya ujenzi wa chujio katika eneo la Tura na kutoa milioni 800 kwa ajili ya hatua za awali za upanuzi wa mradi wa kupeleka maji ya ziwa Victoria katika eneo la Kigwa na jirani.

Shibiti alisema usanifu wa mradi huo umekamilika na wanatarajia utagharimu shilingi bilioni 11 ambapo utasaidia kusambaza maji katima maeneo mbalimbali ya jimbo la Igalula.

Aliongeza kuwa Serikali imeshatenga jumla ya shilingi bilioni 1.3 ambazo zinatokana na mpango wa lipa kulingana na matokeo(P4R) kwa ajili ya kuimarisha miundo mbinu na kuimarisha Jumuiya  10 za watumia Maji yakiwemo ya kutoka ziwa Victoria.

Aidha Meneja huyo wa RUWASA wilayani Uyui alisema wanatarajia kutumia zaidi ya milioni 200 kujenga miundo mbinu ya kusambaza maji katika eneo la Ndono.

No comments:

Post a Comment

Pages