HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

February 05, 2020

Ufaransa yashauri utunzaji Mazingira Ziwa Victoria

Na Irene Mark

WAKAZI wa Afrika Mashariki wanaotumia Ziwa Victoria, wameshauriwa kutunza na kulinda vidaka maji ya ziwa hilo na kuepuka uchafuzi wa mazingira yake.

Nchi zinazotumia zaidi Ziwa Victoria ni Tanzania, Uganda na Kenya.

Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Frédéric Clavier, wakati wa majadiliano kati ya watendaji wa serikali wanaosimamia Ziwa Victoria, wanafunzi 150 wa vyuo vikuu na wadau wa utunzaji wa mazingira ya ziwa na viumbe vilivyomo.

"Nawashauri wanaozunguma ziwa victoria kuwa wa kwanza kulinda rasilimali hiyo Kwa faida yao na kizazi kijacho, watengeneze mikakati bora ya kulitunza lisipotee.

"Taarifa zinaonesha watu zaidi ya milioni 30 wanategemea uwepo wa ziwa Victoria na viumbe wake," alisema Balozi Clavier na kuongeza kuwa changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi na maendeleo ya shughuli za kila za binaadamu zinahatarisha uhai wa rasilimali hiyo.

Majadiliano hayo yaliyohusisha zaidi vijana, yaliandaliwa na Ubalozi wa Ufaransa yakihamasisha utunzaji wa Ziwa Victoria na viumbe vilivyomo kwa kuwa vinasaidia wananchi kupata ajira, chakula na kuchangia pato la taifa.


Hii ni Mara ya pili kwa Ubalozi wa Ufaransa kuandaa na kuongoza mtajadiliana hayo yenye nia ya kutunza mazingira na kuokoa viumbe hai vilivyomo ziwani.

"Tunazingatia sana utunzaji wa mazingira hasa ya Ziwa Victoria ili lisipote ndio maana nchi yangu imetoa msaada wa Dola milioni moja za Marekani kwa miradi ya ekolojia ili kuwafikia wakulima wadogo 8,000 wanaofanya kilimo rafiki wa mazingira.

"Ni mradi wa majaribio kupitia misaada ya kikanda ya Dola milioni 1.5 kutoka Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), lengo pekee ni utunzaji wa mazingira ya Ziwa Victoria kwa kuwekeza zaidi ya Dola milioni 220 kwa miaka 10 ili kufanikisha upatikanaji wa maji na usafi wa mazingira.

Baadhi ya wanavyuo waliiomba Serikali kupitia majadiliano hayo kuwezesha upatikanaji wa vitabu vya na mitaala ya uvuvi na masuala ya maji vinavyokwenda na wakati.

"Tunafundishwa lakini mifano inayotolewa vitabuni inahusu Ulaya na Marekani sio Tanzania wala Afrika lazima tusime mambo yanayotuhusu ili tuweze kujisimamia," alisema Magesa Mussa miongoni mwa wanafunzi walioshiriki majadiliano hayo.

No comments:

Post a Comment

Pages