HABARI MSETO (HEADER)


March 26, 2020

BILIONI 4 KUTAFITI VIRUSI, MALARIA

Mtafiti wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), akiweka sampuli kwenye mashine ya kuchambua vinasaba ya Oxford MinION nanopore. (Na Mpiga Picha Wetu). 

Na Suleiman Msuya
 
TUME ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Mfuko wa utafiti wa Afrika Kusini (National Research Foundation) na Taasisi Oliver Tambo Africa Research Chairs Initiative, inatarajia kuwezekeza Dola za Marekani milioni 2 ambazo ni zaidi na shilingi bilioni 4 katika Chuo Kikuu cha Kilimo (SUA) na Nelson Mandelea Arusha ili kufanya utafiti wa virusi na dawa za malaria.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Utafiti, COSTECH, Profesa Mohamed Sheikh wakati akizungumza na Habari Mseto Blog.
Prof. Sheikh alisema Tanzania inatarajia kupata fedha za utafiti ya kiasi cha dola milioni 2 za Marekani hivyo wamelazimika kuelekeza kwenye utafiti huo ili kuweza kutatua changamoto mbali mbali ndani ya nchi zikiwemo tafiti za magonjwa yanasobabishwa na virusi na malaria.
Alisema magonjwa ambayo yanatokana na virusi yanasumbua duniani kote hivyo ni vema kuwekeza katika utafiti ili kuweza kusaidia jamii.
Sheikh alisema ushahidi ni hali ilivyo sasa ambapo dunia inateswa na kirusi cha corona kinachosababisha ugonjwa wa COVID-19.
“Fedha hizo za utafiti Dola za Marekani milioni 2 zinatolewa na COSTECH, zinatarajiwa kuwekezwa katika vyuo vya SUA na Nelson Mandela ambapo watafiti wetu kwa kushirikiana na Tume wataweza kuja na majibu kuhusu maradhi haya yanayosumbua jamii” alisema.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema SUA watatafiti kuhusu magonjwa yanahusu virusi vinavyosababishwa na wanyama ambavyo vinaweza pia kuathiri afya ya binadamu.
Alisema kwa upande wa Nelson Mandela watajikita katika utafiti wa kupata tiba ya malaria kwa kutumia utaalamu wa nano-technologyambayo itaweza kupunguza au kuondoa changamoto hiyo.
Alisema tume inashirikiana na wadau mbalimbali wa ndani na nje kuratibu utafiti unaowezesha watafiti wazawa ambao wanatatua matatizo ya ndani.
Kaimu Mkurugenzi huyo alisema matarajio yao ni kutumia majibu ya utafiti huo kwa nchi zote hasa za Afrika ambazo zitahitaji ili kuweza kuokoa jamii na magonjwa yanayosabishwa na vurusi na ugonjwa wa malaria.
Prof. Sheikh alisema katika juhudi za kuratibu utafiti wanaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali ikiwemo Kituo cha Kimataifa Uhandisi Jeni na Bioteknolojia (ICGEB), kilicho na makao makuu yake nchini Italia ili kuhakikisha wanabadilisha jamii ya Kitanzania kimaendeleo na uchumi.
Sheikh alisema pia wamekuwa wakipata ufadhili wa masomo katika ngazi ya uzamili na uzamivu katika maeneo mbalimbali katika kada tofauti kama magonjwa ya afya, akili na mengine.
Aidha, alisema wanatumia watafiti waandamizi ambapo wanashindanishwa na nchi mbalimbali ambazo wanashirikiana nazo.
“Ushirikiano wetu na ICGEB umekuwa na manufaa mengi kwa Tanzania ikiwa ni pamoja na watafiti wa kitanzania kupata zaidi ya dola 350,000 za Marekani na huku COSTECH imechangia ada ya uanachama wa dola 5,000 kwa mwaka alisema.
Lengo la Tume ni kutumia uvumbuzi katika nyanja za sayansi na teknolojia ili kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na maisha mazuri na afya njema.

No comments:

Post a Comment

Pages